Panya Road, wazazi wao watiwa mbaroni


Dalila Sharif

JESHI la Polisi Mkoa wa Temeke, linashikilia vijana 14 wa ‘Panya Road’ na wazazi wao 11, likiwatuhumu wazazi kwa madai ya kukiuka sheria ya malezi ya watoto wao.

Pia limeonya kuwa kuanzia sasa litawachukulia hatua kwa kuwashitaki kwa kuficha uovu wa watoto wao.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi wa Temeke, Gilles Murato alisema ‘Panya Road’  wanashikiliwa kwa kujihusisha na uvamizi kwenye Tamasha la Kuinua Vipaji lililoandaliwa na Clouds Fm  na kupora wananchi kwa kuwashambulia baadhi yao na kuwajeruhi.

Alisema kwa mujibu wa sheria hiyo ya watoto ya mwaka 2009 vifungu vya 7 na 9 wazazi na walezi wana wajibu wa kulea watoto wao kwenye mazingira mazuri, ambayo hayatawasababishia madhara kisaikolojia, udhalilishaji na kuhakikisha wanapata mahitaji ya elimu, afya na mavazi.

Kutokana na wazazi hao kukiuka sheria hiyo, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya na kwa mujibu wa kifungu cha Sheria namba 14, mzazi atakayeshindwa kutekeleza  kifungu 7-9 hicho atafikishwa mahakamani na akitiwa hatiani atapewa adhabu ya kifungo cha miezi sita jela au kulipa faini ya Sh milioni tano.

"Tunashukuru wananchi wa Buza kwa kutupa ushirikiano wa kukamata wahalifu hawa, tunaomba waendelee na ushirikiano huo kwa Polisi ili kukabiliana na vijana hao ambao wamekuwa wakifanya vitendo viovu dhidi ya raia," alisema Murato.

Wazazi waliofikishwa kituoni hapo, walisema wanasikitishwa na tabia za vijana wao kujiingiza kwenye makundi ya kihalifu huku wakisema hawakuwa wakijua kama watoto wao ni ‘Panya Road’.

Enesto Chalo ambaye ni mmoja wa wazazi hao, alisema alishangazwa kupewa taarifa ya mtoto wake kuuawa kwa kipigo cha wakazi hao, baada ya wananchi kumgundua kuwa mmoja wa kundi hilo la wahalifu.

"Nimesikitishwa na kitendo cha mtoto wangu, Issack Ernesto (16) kujiingiza kwenye kundi hilo na kupewa taarifa kuwa amekufa, lakini alizinduka akiwa mochari," alisema Chalo.

Salumu Ally alisema mtoto wake ni mmoja wa wanaoshikiliwa kwa uhalifu wa kundi hilo, hivyo alisikitishwa na tabia ya mtoto huyo kujiingiza kwenye kundi hilo hali nyumbani anaonekana mtiifu.

"Kwa kweli tabia ya kujihusisha na kundi hili ni hali inayomsababishia mzazi ugonjwa wa moyo kutokana na mwenendo ambao mtoto huyu anaufanya bila wazazi kujua," alisema Ally.

Watuhumiwa hao walikiri mbele ya waandishi wa habari kujihusisha na makosa hayo kwa kujiingiza kwenye kundi hilo la ‘Panya Road’ na kuonesha baadhi ya silaha walizokuwa wanatumia kufanyia matukio ya kihalifu.

Tukio hili si la kwanza kutokea Temeke hali inayosababisha baadhi ya wakazi kuishi kwa woga, hivyo Jeshi hilo liliwataka wakazi hao kushirikiana  nalo kutoa taarifa za uhalifu unaojitokeza.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo