CUF halali kumburuta Msajili Kortini


Grace Gurisha

WAKATI mgogoro ndani ya CUF ukiendelea kutishia mpasuko mkubwa, Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam imeiruhusu Bodi ya Wadhamini ya Chama hicho kufungua kesi ya msingi dhidi ya uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.

Bodi hiyo inaiomba Mahakama hiyo kufuta uamuzi Msajili, Jaji Francis Mutungi wa kumtambua Profesa Ibrahim Lipumba kama Mwenyekiti wa Chama hicho. Hivi karibuni, Ofisi ya Msajili ilitoa msimamo na ushauri wake kuhusu mgogoro ndani ya CUF, ikielezea kumtambua Profesa Lipumba kuwa Mwenyekiti halali wa Chama hicho huku ikishauri anayepinga hili kwenda mahakamani.

Jana, Bodi hiyo ilipata ruhusa ya kufungua kesi hiyo wakati chama hicho kikiwa bado kwenye mgogoro na mgawanyiko, upande mmoja ukimwunga mkono Mwenyekiti Lipumba na mwingine ukimpinga kwa madai kuwa si halali kutokana na kujiuzulu awali na kurejeshwa na Msajili wa Vyama vya Siasa.

Bodi hiyo ilifikia hatua hiyo, kwa sababu haimtambui Profesa Lipumba kama Mwenyekiti, kwa hiyo anachokifanya Jaji Mutungi ni kukiuka sheria na tararibu zilizopo. Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Ama –Isario Munisi wa Mahakama hiyo, baada ya kupitia nyaraka zilizotolewa na Bodi hiyo na hati ya kiapo cha Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad na kuridhia wafungue kesi hiyo.

Jaji Munisi alisema sababu za kupokea nyaraka hizo za maombi ya kufungua kesi, ni kutokana na kupitia nyaraka hizo za maombi na kuona kuwa ziko sahihi, hivyo wanapaswakufungua kesi hiyo ndani ya siku 14 ikiwa na hoja muhimu wanazobishania.

Baada ya maombi hayo kukubaliwa kwa kupewa kibali hicho, Wakili wa Bodi hiyo, Juma Nassoro alidai kuwa kisheria wanatakiwa wafungue kesi hiyo ndani ya siku 14, lakini wao watafungua ndani ya siku saba ili kesi hiyo isikilizwe na kutolewa uamuzi haraka.

“Tunatarajia ndani ya siku saba tutakuwa tumefungua kesi ili iweze kutoa nafasi ya kuanza kusikilizwa kwa kesi ya msingi,” alisema Nassoro. Mbali na Jaji Mutungi na Profesa Lipumba, pia kuna wanachama 12 ambao nao wamefunguliwa kesi na Bodi hiyo kwa madai ya kukiuka taratibu zilizowekwa na chama hicho.

Awali, Bodi hiyo iliwasilisha mahakamani hapo maombi ya kutaka Mahakama itoe amri ya kumzuia Msajili kuingilia masuala y ndani ya chama hicho. Nassoro alisema jukumu la kufungua kesi hiyo alipewa na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif.

Alisema ilifikia hatua hiyo ya kufungua kesi kutokana na mgogoro unaoendelea, kwa sababu kuna taratibu na sheria zimekiukwa za kuongoza chama.

Nassoro alisema wanaiomba Mahakama itoe amri ya kumzuia Jaji Mutungi kufanya kazi nje ya mamlaka yake, kwa kuvunja kanuni na taratibu za kazi yake kinyume na sheria inayomwongoza kama Msajili. Alisema anachokifanya Jaji Mutungi ni kuingilia demokrasia ya wananchi jambo ambalo si sahihi. Katika suala la sharia, Msajili hana mamlaka ya kuengua au kubatilisha uamuzi wa vyama.

Nje ya Mahakama

Pia chama hicho kimemwonya Jaji Mutungi kutojihusisha na masuala ya CUF, ikiwamo kuandika barua benki kumruhusu Profesa Lipumba kufungua akaunti kwa ajili ya ruzuku.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa CUF Taifa, Twaha Taslima alisema wanaishukuru mahakama hiyo kwa kutoa ruksa ya kuwasilisha maombi yao ya kesi. Taslima ambaye pia na Mwanasheria wa chama hicho, alisema kwa sasa wanachama wa CUF na wananchi wanapaswa kutuliza nyoyo zao kwa sababu mgogoro huo umefika kwenye mikono ya sheria.

“Tunawaambia haki lazima itatendeka na Mahakama itaona ni akina nani walionayo, hivyo hatutaki misukosuko ndani ya chama chetu,” alisema.

Mtatiro

Mwenyekiti wa Kamati ya Muda ya Uongozi wa CUF, Julius Mtatiro alitoa onyo kwa Jaji Mutungi dhidi ya kujihusisha na harakati za chama hicho kinyume na sharia ya vyama vya siasa inavyosema.

Alisema wamesikitishwa na barua ya Jaji Mutungi kwenda benki mbalimbali ikiwamo NMB tawi la Ilala kwa ajili ya kufungua akaunti nyingine ya chama huku akifahamu kikatiba hairuhusiwi.

Alisema tayari chama hicho kimebaini njama za kuandaa nyaraka batili zinazofanywa na Lipumba na Msajili kwa ajili ya kufungua akaunti nyingine baada ya kukataliwa na NMB.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo