CCM: Hatuna mpango kuzungumza na CUF


Is-haka Omar, Zanzi bar

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), hakina mpango wa kufanya mazungumzo au makubaliano na CUF kuhusu uchaguzi uliopita.

Msimamo huo ulitolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai wakati akijibu hoja za Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CUF, Ismail Jussa Ladhu kwenye mahojiano maalumu na gazeti moja nchini juzi.

Alisema uchaguzi umekwisha, kazi iliyo mbele ni kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/20 ili kuhakikisha ahadi zilizotolewa kwenye kampeni za uchaguzi mkuu zinatekelezwa kwa vitendo.

Vuai alisema Jussa alinukuliwa akisema CUF inaangalia uwezekano wa kufanya mazungumzo na CCM kuhusu uchaguzi, jambo ambalo CCM haiko tayari kukaa meza moja na chama hicho kujadili jambo ambalo lilishafanyiwa uamuzi halali kwa mujibu wa kanuni, taratibu na sheria za nchi.

Alisema chama hicho kinaweza kukaribisha chama chochote cha upinzani kuzungumzia kuimarisha na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM na si uchaguzi mkuu ambao ulipita kisheria na serikali zinaendelea kutumikia wananchi kwa uadilifu.

Alisema kujadili serikali za Zanzibar na Tanzania hivi sasa ni kwenda kinyume na sheria za nchi kwani zimetokana na uamuzi halali wa wananchi kupitia uchaguzi wa kidemokrasia.

Alitaka wafuasi wa CCM na wananchi kupuuza madai ya kiongozi huyo hasa mantiki ya kuundwa kwa Serikali ya Mpito Zanzibar, hatua ambayo alisema haiwezekani na inaashiria kuvunja Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Pia alisema hoja na ajenda ya kufanyika uchaguzi wa mpito Zanzibar ni ndoto au kujifurahisha kwa kutafuta umaarufu wa kisiasa usio na uzani wala mafanikio kwa wafuasi wa chama kinachojenga hoja hizo nchini.

Naibu Katibu Mkuu huyo, alifafanua kuwa CUF imekosa mwelekeo na ndiyo maana viongozi wake wanadanganya wafuasi wao kwa mambo ambayo kiuhalisia wanajua hayawezekani kisiasa Zanzibar.

Alisema jukumu la msingi linalotekelezwa na CCM sasa ni uhakiki wa mali zake ili kujiridhisha zaidi kama mkakati wa uimarishaji hali ya siasa na uchumi ndani ya CCM.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo