Walinzi SGA wadaiwa kuibia TATA Holdings


Jemah Makamba

WALINZI wa kampuni ya SGA wamefikishwa kwenye Mahakama ya Wilaya ya Ilala wakituhumiwa kula njama, kuvunja na kuiba ya vitu venye thamani ya Sh milioni 197 mali ya kampuni ya TATA Holdings Tanzania Ltd.

Watuhumiwa hao ni Godfrey Gosbert (23), James Edward (26), Ubaya Simba (33), Michael Moses (26), Musa Mukaubani (22) na Halfan Mohamed (35).

Akisoma mashitaka hayo jana mbele ya Hakimu Adelf Sachore, mwendesha mashitaka Florida Wenceslaus alidai kuwa Desemba mwaka jana washitakiwa walikula njama kwa nia ya kuiba.

Ilidaiwa pia Mahakamani hapo kuwa Desemba 13 mwaka jana, washitakiwa wakilinda ghala la kampuni hiyo, walivunja kwa nia ya kuiba.

Katika hatua nyingine, ilidaiwa kuwa Desemba 13 usiku walivunja na kuiba vitu mbalimbali zikiwamo zana za kilimo na mbolea zote zikiwa na thamani ya Sh milioni 197.

Hata hivyo, mwendesha mashitaka alidai kuwa washitakiwa wote kwa pamoja walishitakiwa kwa kosa lingine la kushindwa kuzuia uhalifu dhidi ya Kampuni hiyo iliyopo barabara ya Nyerere wakiwa kama walinzi.

"Sina kipingamizi na dhamana kama washitakiwa watakidhi masharti kwani kosa lao linadhaminika," alisema Wenceslaus.

Hakimu alisoma masharti ya dhamana ikiwa ni wadhamini wawili wanaofanya kazi katika taasisi inayofahamika na mmoja awasilishe hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh milioni 32 na kusaini ahadi ya Sh milioni 32.9.

Washitakiwa waliita wadhamini wao lakini hakuna aliyekidhi masharti ya dhamana hakimu akasema kesi hiyo itatajwa Januari 16, washitakiwa wote wakarudishwa rumande.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo