DC wa Uyui, haki na hatari ya ‘kufa’ kisiasa



Mashaka Mgeta

Mashaka Mgeta
SI jambo la kawaida kutokea kiongozi wa kuteuliwa na Rais, akajiuzulu nafasi yake ili akafanye shughuli binafsi, isipokuwa kutokana na kashfa zinazoiathiria jamii pana hasa katika upatikanaji wa huduma za kijamii.

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Uyui mkoani Tabora, Gabriel Mnyele, ametangaza kuachana na kazi hiyo, baada ya kumuandikia barua Rais John Magufuli, akiomba ombi lake likubaliwe akafanye shughuli binafsi.

Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu imethibitisha kujiuzulu kwa Mnyela na kwamba Rais John Magufuli alilikubali ombi hilo. Hivi sasa Mnyele ambaye ni mwanasheria anarejea kwenye shughuli binafsi ambazo si lazima umma kuzijua, kwa maana hayupo tena katika utumishi wa umma.

Pamoja na Mnyela, ninatambua kuwapo wateuliwa wengine waliowahi kufukia hatua kama ya Mnyele, muda mfupi baada ya kuteuliwa kwao. Miongoni mwa hao ni aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Ally Masoud Maswanya, akajiweka kando kushika wadhifa huo hata kabla ya kuapishwa.

Matukio hayo mawili na mengine yanayofanana na hayo, yanaweza kuwa moja ya vigezo vinavyoweza kubatilisha hisia hasi juu ya hatua iliyofikiwa na Mnyele.

Lakini katika ujumla wake, utumishi wa umma unapasa ‘kutawaliwa’ na utayari wa mtu ‘kujikana’ mwenyewe, kujiondoa katika kuyatafuta yaliyo ya binafsi na badala yake kujielekeza zaidi kwenye masuala ya kulitumikia taifa na kuwahudumia watu.

Nadharia hiyo inatoa nguvu ya sababu zinazotajwa kuwa kishawishi kwa Mnyele kujiuzulu, kwamba anataka kujihusisha na masuala binafsi. Nafsi inapomtuma mtu kuyafanya yanayokidhi matakwa binafsi, anapaswa kusikilizwa na kupewa fursa hiyo.

Vinginevyo, kuendelea kuwapo madarakani kimwili huku fikra zake zikijikita katika kutafuta na kuendeleza masuala binafsi, ndipo kunapotokea mgongano wa maslahi. Mhusika anabaki kuwa katika mapambano dhidi ya matamanio ya nafsi yake.

Kwa bahati mbaya, si katika Tanzania bali nchi nyingi hasa zinazoendelea, baadhi ya viongozi wa umma wamekuwa wakitumia nyadhifa walizonazo kama nyenzo ya kuyafikia maslahi binafsi.

Wanajitoa katika kuyafikiri na kuyafanyia kazi yaliyo yenye manufaa kwa umma, badala yake wanatumia fursa za kuwamo katika utawala ili kuyafikia mahitaji na matamani yao binafsi.

Hivyo, Mnyele anapojizulu kupitia sababu ya kupata fursa pana ya kushughulika na masuala binafsi, maana yake rahisi ni kwamba ameuepuka mgongano wa maslahi. Kwamba angeweza kubaki kulitumikia taifa akiwa Mkuu wa Wilaya huku nafsi yake ikiwa katika matamanio ya kuyafikia mafanikio binafsi.

Kuyatafuta na kuyafikia mafaniko binafsi si dhambi kwa mtu, maana kila mwenye nafsi anapaswa kustawisha maisha yake, ya familia, ndugu, jamaa na taasisi alizo mshirika kama dhehebu la dini anaposali na kuabudu.

Kwa hiyo Mnyele alipoisikia sauti ikimhitaji kujiweka kando dhidi ya fursa ya kuwa Kiongozi wa umma aliye mwakilishi wa Rais wa nchi katika ngazi ya wilaya, anastahili pongezi, ameendeleza kudhihirisha namna taifa linavyoendeleza misingi ya haki zinazotokana na uhuru wa mtu kufanya uamuzi usiokinzana na matakwa ya sheria.

Isingekuwa rahisi kwa taifa lenye utawala wa kidikteta kumuacha Mkuu wa Wilaya anayetumia kigezo cha matakwa binafsi kutoka katika kuwaongoza watu, atimize nia hiyo pasipo kujali athari kwa uchumi, utawala na uongozi.

Viongozi wa umma wanapaswa kufikiria asili ya nafasi walizokabidhiwa kama dhamana, iwe kwa njia ya kupigiwa kura na wananchi, kuteuliwa ama kuajiriwa. Haifai kwa viongozi wa umma kung’ang’ania madarakani ama katika uongozi hata pale wanapojitambua kwamba hawafai kulitumikia taifa kwa mujibu wa dhamana waliyopewa.

Pamoja na taswira hiyo inayolenga uadilifu katika utumishi wa umma, kutumia uhuru wa kujieleza na kujiweka kando dhidi ya mgongano wa maslahi, kuna uwezekano Mnyele akawa katika mazingira magumu ya kisiasa.

Atakuwa katika mazingira magumu ikiwa ataendeleza ndoto za kujiimarisha zaidi kisiasa baada ya ‘kutia nia’ ya kuwania ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka juzi.

Hata hivyo Mnyele alishindwa katika kura za maoni na hatimaye Sebastian Kapufi akashinda katika kura za maoni na kwa Uchaguzi Mkuu, hivyo kuwa Mbunge.

Hoja itakayoibuliwa ikiwa Mnyele atahitaji tena kuwania ubunge, ni pamoja na dhamira iliyomtuma kujiondoa ndani ya mfumo wa kuwatumikia wananchi. Kwamba kama sababu ya kwenda kufanya shughuli binafsi itakuwa msingi wa kujiuzulu kwake, ataaminika vipi ikiwa atataka kuwania nafasi kama ubunge?

Pili, kama ameteuliwa na Rais John Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, akajizulu kutoka nafasi muhimu katika utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama hicho, je, ataaminika katika nafasi gani nyingine inayompa fursa ya kuchangia maendeleo yenye kuimarisha imani ya wananchi wengi kwa chama hicho?

Lakini kwa ujumla wake, Mnyele amejiuzulu nafasi yake kwa sababu zinazotajwa, hivyo kuwa mfano kwa wengine wakiwamo wasioendana na kasi ya Rais Magufuli. Kila la heri!

Mashaka Mgeta- 0754691540
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo