TSN yatakiwa kubeba ajenda za Serikali


Salha Mohamed

WAZIRI wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye amelitaka Shirika la Magazeti ya Serikali (TSN) kubeba ajenda za Serikali ya Viwanda.

Aidha, Rais John Magufuli ameahidi kutembelea ofisi za magazeti hayo kwa kushitukiza ili kuona utendaji kazi wao.

Nape alisema hayo Dar es Salaam jana kwenye maadhimisho ya miaka 10 ya gazeti la Habari Leo.

Alisema shauku yake ni kuona gazeti hilo likibeba ajenda za Serikali Viwanda.

“Ningetamani mbebe ajenda za Serikali kama Serikali ya Viwanda, kwa kuhusisha wananchi moja kwa moja,” alisema Nape.

Alisema asilimia 80 ya wananchi ni wakulima, hivyo wanapaswa kuwaaminisha kuwa fursa ya viwanda ni yao na si ya Serikali.

Aliongeza kuwa kupitia gazeti lao, wanatakiwa kudumisha utamaduni na sanaa kwani tayari kuna utamaduni ambao unaanza kupotea.

“Mjali haki za watumishi, muwe wasikivu kwa mambo yao, msiyapuuze muwasikilize na kuwatendea haki…mkiwajali hawa mtapata baraka za Mungu,” alisema.

Aidha, Nape aliwataka kuwa wabunifu na kuongeza motisha kwa wafanyakazi.  

Awali, Mhariri Mtendaji wa TSN, Dk Jim Yonazi alisema mbali na mafanikio waliyopata katika miaka kumi ya gazeti hilo wamejizatiti kutoa yale jamii inayoyataka.

“Kuelekea miaka kumi ijayo, gazeti letu litabadilika kuwa kampuni ya ushauri na kutengeneza fedha nyingi na si tu kuchapisha magazeti,” alisema.

Gazeti la Habari Leo lilisaini makubaliano ya kukuza Lugha ya Kiswahili na Baraza la Kiswahili Tanzania (Bakita) na kuzindua bahati nasibu ya watoto waliozaliwa au kutimiza miaka kumi Desemba 21.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo