Uwakita: Ichunguzeni kwanza nembo ya Halal


Hussein Ndubikile

UMOJA wa Wainjilisti Kikristo Tanzania (Uwakita) umeishauri Serikali kufanya uchunguzi wa uhalali wa matumizi ya nembo ya halal katika bidhaa za vyakula kama inakidhi matakwa ya Katiba na sheria za nchi.

Aidha, umoja huo umesema ubora wa bidhaa za vyakula vya viwandani husimamiwa na Serikali na kuthibitishwa uhalali wa matumizi yake kwa binadamu na Mamalaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Shirika la Viwango nchini (TBS).

Hatua hiyo imekuja baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu nchini (Bakwata), Sheikh Suleiman Lolila mwaka jana, kutangaza kuwa mwaka huu nchi itaanza kunufaika sababu iko mbioni kuingia kwenye orodha ya nchi ambazo bidhaa zake za chakula zitawekwa nembo hiyo na kuuzwa katika mataifa 33.

Akizungumza na gazeti hili, Mjumbe wa umoja huo, Elieza Shinza alisema kitendo cha baraza hilo kusisitiza matumizi ya nembo hiyo ni kuingilia majukumu mamlaka hizo na kwamba endapo itaruhusiwa kutumika inaweza kusababisha ubaguzi wa kiimani na kuleta mgawanyiko katika jamii.

“Kuhusu nembo ya halal mpaka sasa hakuna ushahidi wa kampuni yoyote iliyokataliwa kuuza bidhaa zake nje sababu ya kukosa nembo hiyo kwa msingi huo madai ya Bakwata si ya kweli kwani wanajua uhalali wa mamlaka hizi zote,” alisema.

Alisema endapo Serikali itaruhusu nembo hiyo itumike itakuwa inakiuka Katiba ya nchi  ibara ya 13 ambayo inasisitiza usawa wa watu wote mbele ya sheria na kukataza ubaguzi wa aina yoyote.

Alisisitiza kuwa ibara hiyo katika kifungu cha nne inapiga marufuku mtu yeyote kubaguliwa na mtu au mamlaka yoyote inayotekeleza madaraka yake chini ya sheria yoyote au katika utekelezaji wa shughuli ya mamlaka ya nchi.

Aliongeza kuwa ni vyema Serikali ikatupilia mbali matumizi nembo hiyo kwani ikiruhusiwa itakiuka Sheria ya TFDA na TBS.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo