TUCTA yapigania sheria ya kima cha chini


Laonce Zimbandu

Dk Yahya Msulwa
SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) limesema litapigania   sheria ya kulipwa kima cha chini cha mshahara kinachomwezesha mfanyakazi kumudu mahitaji.

Sheria ya kima cha chini haizingatii kumwezesha mfanyakazi wa ngazi ya chini kumudu mahitaji muhimu ya maisha, ikiwamo chakula, malazi, matibabu na elimu kwa watoto.

Hivyo, kima cha chini kinachomwezesha mfanyakazi kumudu mahitaji ni Sh 750,000 au  zaidi  badala ya Sh 315,000 kiilichotangazwa mwaka 2006.

Katibu Mkuu wa Tucta, Dk Yahya Msulwa, alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam kuhusu vipaumbele vya utendaji wa Tucta mwaka huu.

Alisema tangu mwaka 2006 Tucta ilifanya utafiti kujua kima cha chini cha mshahara kinachomwezesha mfanyakazi kumudu maisha kuwa ni Sh 315,000 kwa mwezi na Serikali ikaombwa isikate kodi, lakini hilo halikufanyika.

“Kuanzia mwaka 2014 mshahara  wa Sh 750,000 ulitakiwa usikatwe kodi ili kupunguza uwiano wa makato ya kodi ya mishahara kwa ngazi zingine, hivyo kodi isizidi kiwango cha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni asilimia 18,” alisema.

Dk Msulwa aliiomba Serikali kupunguza utitiri wa mifuko ya hifadhi ya jamii ili kupunguza gharama za uendeshaji na kuondoa tofauti ya mafao kati ya mifuko hiyo kwa wanachama.

Alisema Tucta inaomba mifuko hiyo ipungue na kubaki miwili yaani mfuko wa watumishi wa umma na mfuko wa hifadhi ya jamii kwa watumishi wa sekta binafsi.

Taaluma

Dk Msulwa alisema Serikali inapaswa kuangalia namna ya kulinda wataalamu wa elimu ya kati, ikiwamo vyuo vya Stashahada ya Ufundi ambavyo vimegeuzwa kuwa vyuo vikuu, hivyo uzalishaji wa wataalamu wa ngazi ya kati kupungua.

Alisema ni ajabu kuzungumzia wataalamu wenye Shahada na Shahada za Juu huku  wakisahau kuwa kila mhandisi anatakiwa kuwa na wataalamu wanne wenye Stashahada huku mwenye Stashahada akitakiwa kuwa na wataalamu kati ya sita na 10 wenye  cheti.

Alishauri siasa isifunike utaalamu kwa vile maendeleo hayawezi kupatikana bila kuhusisha wataalamu katika maeneo mbalimbali, ikiwamo utungaji wa sera na utoaji uamuzi.

Adhabu

Tucta imesisitiza kuwa utoaji adhabu kwa watumishi wa umma kwa makosa mbalimbali yanapaswa kuzingatia sheria zinazotawala mambo ya kazi na ajira, ikiwamo kushirikisha mamlaka zao.

Watumishi wanapaswa kupewa fursa ya kujieleza kwenye Bodi au Tume iundwe kwa ajili ya kuchunguza ukweli wa kosa ili hatua ichukuliwe.

“Itakuwa si busara kwa kila kiongozi hata kama hana mamlaka ya kutoa adhabu akaagiza adhabu bila kufuata taratibu,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo