Makonda aja na mita kwenye teksi


Salha Mohamed

Paul Makonda
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ametaka madereva teksi kuwa na mita ya kuonesha umbali wa safari ya mteja ili alipe kulingana na umbali huo na si kukadiria.

Makonda alisema hayo jana alipokutana na madereva teksi wa Ilala ili kujadili namna bora ya kuboresha huduma hiyo.

Alisema lengo ni kutoa huduma bora za usafiri kama Marekani na Afrika Kusini na kumfanya mteja ajue bei kuliko kukadiria huku akiahidi kuondoa teksi bubu.

"Azma ya Serikali ni kuboresha huduma za usafiri na kuwa wa kipekee, ili kukamilisha hilo nataka teksi zote kutumia vifaa maalumu vitakavyoonesha umbali anaokwenda abiria,” alisema.

Aliongeza kufanya hivyo kutaondoa gharama za ukadiriaji na kusaidia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwatoza kodi stahiki sambamba na kuweka rangi na namba kwenye magari ili yatambulike.

Alisema ili kuboresha huduma ya usafiri huo, ni lazima wahakikishe wanajadili mfumo bora wa uendeshaji wa biashara zao kwa manufaa yao na abiria.

"Nawapa wiki moja mjadiliane na mkija hapa mje na majibu ya kutatua kero zenu na namna bora ya kuendesha biashara zenu bila bughudha," alisema.

Makonda alitaka madereva hao kuwa na utamaduni wa kutoa taarifa wanapohisi abiria anajihusisha na matukio ya kihalifu ili Taifa liwe salama.

"Tutaondoa teksi bubu zote, yeyote atakayezitumia akumbuke akikumbwa na tatizo hakuna atakayemsaidia, tutaendeleza mfumo wa kupaka rangi na kutoa namba kwa teksi zote ili kuhakikisha huduma zinakuwa bora," alisema.

Makamu Mwenyekiti wa Madereva wa Teksi wa Ilala, Jacob Anyandwile alisema miongoni mwa changamoto wanazokutana nazo ni kodi kubwa za TRA, uwepo wa huduma ya teksi kwa njia ya mtandao unafanywa na kampuni ya UBA.

Alisema UBA imewaharibia soko kwani kampuni hiyo inatoza bei ndogo zaidi ikilinganishwa na wao huku gharama za uendeshaji zikiwa hazilingani, kwani hulipa kodi ndogo.

Aidha, alisema uwepo wa bajaji kinyume na utaratibu, wamachinga kupanga bidhaa zao barabarani ni baadhi ya mambo yanayosababisha kutofika kwa wakati maeneo wanakopeleka abiria.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo