Mkuu wa Wilaya abwaga manyanga


Odace Rwimo, Uyui

Gabriel Mnyele
MKUU wa Wilaya ya Uyui mkoani Tabora, Gabriel Mnyele, amejiuzulu.

Mnyele ambaye ni Mwanasheruia kwa taaluma jana alipita kila idara za Halmashauri ya Wilaya hiyo kuaga akianzia kwa watumishi wa ofisi yake.

Taarifa za awali zilisema kuachia kwake ngazi ya ukuu wa wilaya kulitokana na kutingwa na majukumu binafsi aliyonayo.

Aidha, imedaiwa kuwa Mkuu huyo aliandika barua mwaka jana akiomba kujiuzulu nafasi hiyo.

Taarifa zaidi zilisema baada ya kuandika barua alijibiwa na mamlaka ya uteuzi akikubaliwa kuachia nafasi hiyo.

Hata hivyo, Mnyele alipoulizwa jana kuhusu taarifa hizo huku akicheka, alisema: “Mimi bado nipo ofisini na leo nimehudhuria kikao cha ulinzi na usalama. Lakini kwa nini msiulize mamlaka ya uteuzi?”

Baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo ambao hawakutaka kutajwa majina walisema  jana kuwa Mkuu huyo alipita kila idara akianzia ofisi mwake kuaga.

“Bosi wetu alianzia ofisini kwake kuaga watumishi na baadaye alipita kila idara na kubwa ambalo alikuwa akieleza ni uamuzi alioufanya bila shinikizo,” alisema mmoja wao.

Alisema aliwambia uamuzi wa kusitisha ajira yake hautokani na kushindwa kasi ya Rais Dk John Magufuli bali anataka kufanya kazi zake binafsi.

“Alisema majukumu binafsi yamembana na ndiyo maana kafikia uamuzi huo na si vinginevyo kama watu wanavyoweza kufikiria,” alisema mtumishi huyo wa Halmashauri.

Aidha, inadaiwa aliwaeleza anaachia ili wengine washike nafasi hiyo ila ataendelea kushirikiana na wana Uyui.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Hadija Makuwani alilieleza gazeti hili kuwa bosi wake huyo alimuaga asubuhi jana kwa maelezo kuwa amesitisha ajira yake kwa hiari ili akafanye shughuli zake.

Aliongeza kuwa kwa sasa wanasubiri kuletewa Mkuu mwingine wa Wilaya ili aendelee kutekeleza majukumu yao ya kuwaletea maendeleo wananchi wao.

Gazeti hili lilimtafuta Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri ili kupata maoni yake lakini simu yake ilikuwa haipatikani muda wote hadi tunakwenda mtamboni.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo