Mokiwa bado ni askofu—Msemaji


Leonce Zimbandu


Askofu Valentino Mokiwa
MSEMAJI wa Askofu Valentino Mokiwa wa Kanisa la Anglican Dayosisi ya Dar es Salaam, Yohana Sanga amesema kanisa hilo litaendelea kuongozwa kwa kuzingatia vikao halali vitatu, kikiwamo kikao cha nyumba ya maaskofu ambacho ni chombo kinachotoa dira na mwelekeo wa kanisa.

Kikao kingine ni wajumbe wa sinodi pamoja na Kikao cha Halmashauri ya Kudumu ya Kanisa, hivyo maamuzi yatakayotolewa katika vikao hivyo ndiyo yatakayozingatia taratibu za kanisa.

Sanga aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na gazeti hili katika Kanisa la Mtakatifu Albano lililopo eneo la Posta jijini Dar es Salaam jana.

Alisema Askofu Valentino Mokiwa ataendelea kuwa Askofu wa Jimbo la Dar es Salaam, licha ya taarifa kwamba hatajihusisha tena na huduma.

Aliongeza kuwa Askofu Mokiwa hana mipaka ya eneo la kuabudu kwa sababu makanisa ya Anglican jijini Dar es Salaam yapo chini ya uangalizi wake.

“Leo (jana) sijawasiliana na Askofu huenda amekwenda kuabudu kanisa jingine, lakini jimbo halina taarifa rasmi na kile kilichotangazwa kwenye vyombo vya habari bali Mokiwa bado ni Askofu wa Jimbo la Dar es Salaam,” alisema.

Alisema sakata hili limeanza muda mrefu, kwani Askofu Mkuu wa Anglican Tanzania, Askofu Jacob Chimeledya aliandika waraka wa kumtaka Askofu Mokiwa ajiudhuru, baada ya kanuni kutozingatiwa uamuzi huo ulishindikana.

Imedaiwa kuwa chanzo cha mgogoro huo ni baada ya Askofu Valentino Mokiwa kuhamisha Mapadre kutoka kanisa moja kwenda jingine, hivyo mmoja wa Mapadre hao aligoma kuhama.

Hali hiyo ilimlazimu Askofu Mokiwa kumvua upadre, hata hivyo aliendelea kukaidi hatua hizo zilizochukuliwa na Askofu wa jimbo na kupelekea kiongozi huo kwenda kutoa malalamiko kwa Askofu Mkuu wa Kanisa hilo mjini Dodoma.

Haijafahamika kama vikao halali vya maamuzi vya kanisa hilo vimekaa na kujadili changamoto hiyo kabla ya kutoa maamuzi au la, hivyo kila muumini wa kanisa hilo bado haelewi hatima ya mvutano huo ndani ya kanisa.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo