Ubunge wa Bulembo na Kabudi shakani


*Wanasheria wasema uteuzi wao wapingana na Katiba
*Kifungu chasisitiza idadi ya angalau wanawake watano

Fidelis Butahe

Profesa Palamagamba Kabudi
NANI atatoswa? Ndilo swali la kujiuliza kutokana na ubunge wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Abdallah Bulembo na nguli wa sheria, Profesa Palamagamba Kabudi wanaosubiri kuapishwa baada ya kuteuliwa na Rais John Magufuli, kuwa shakani kutokana na uteuzi wao kutoendana na Katiba.

Bulembo na Kabudi waliteuliwa Jumanne kuwa wabunge na hivyo kusubiri kuapishwa katika Mkutano wa Sita wa Bunge utakaoanza Januari 31 mwaka huu, lakini kabla ya kuapishwa, imebainika kuwa uteuzi wa mmoja wao unapingana na Ibara ya 66 (1) (e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kifungu hicho cha Katiba kinasema uteuzi wa Rais wa nafasi 10 za wabunge, angalau watano wanapaswa kuwa wanawake.

“Wabunge wasiozidi kumi walioteuliwa na Rais kutoka miongoni mwa watu wenye sifa zilizotajwa  katika aya ya (a) na (c) za uibara ya 67 na angalau wabunge watano kati yao wakiwa wanawake,” inasema Ibara hiyo ya Katiba ya mwaka 1977.

Kutokana na kifungu hicho wanasheria waliozungumza na gazeti hili walisema kuapishwa kwa Bulembo na Profesa Kabudi, kutakiuka kifungu hicho cha Katiba kwa sababu mpaka sasa Rais ameteua wabunge wanane, huku wawili tu wakiwa ndio wanawake huku zikiwa zimebaki nafasi mbili za uteuzi.

Walisema kutokana na masharti hayo ya Katiba, hata akiteua wanawake katika nafasi hizo mbili, bado hawatafikia watano, na kusisitiza kuwa uapisho wa mmoja wa wateule hao au wote, utapaswa kusitishwa ili kulinda kiapo cha Rais, Spika wa Bunge na Katibu wa Bunge cha kuilinda na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Walisema mbali na kuwa kinyume na Katiba, huenda kuapishwa kwao bungeni kukazua mvutano mkali kutoka kwa wabunge, kwa sababu wawakilishi hao wa wananchi watatumia Katiba ya nchi kupinga jambo hilo.

Tayari Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) limeibuka na kueleza kusudio la kufungua kesi mahakamani kwa hati ya dharura, kupinga uteuzi huo, kwa sababu ni kinyume na Katiba, likiitaka Mahakama itoe tafsiri ya kisheria.

Wateule

Tangu alipoingia madarakani Novemba 5 mwaka juzi, Rais Magufuli ameshateua wabunge wanane, wakiwamo Bulembo na Profesa Kabudi.

Wawili ni wanawake ambao ni Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson na Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako.

Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Augustino Mahiga, Profesa Makame Mbarawa (Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano), Dk Philip Mpango (Fedha) na Dk Abdallah Posi  ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu.

Wanasheria

Kwa masharti ya kutotajwa gazetini kwa maelezo kuwa wateule hao ni watu wake wa karibu, mmoja wa wahadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Kitivo cha Sheria alisema:

“Katiba inasema wasiteuliwe wanaume zaidi ya watano, maana yake angeweza kuteua wanawake hata saba na wanaume watatu. Wanaume hawapaswi kuzidi watano, ila wanawake wanaweza hata kuzidi watano.”

Alisema wateule hao watakapoapishwa bungeni, wabunge wanaweza kuwasilisha hoja ya kutaka wasiapishwe, ili uteuzi huo urejeshwe kwa Rais sambamba na tamko kuwa kiongozi mkuu wa nchi amekiuka Katiba, lengo likiwa ni kumtaka apitie upya uteuzi huo.

“Nadhani ndicho kitakachofanyika. Hapo ni wazi kuwa Rais amevunja Katiba. Wakienda kuapishwa, Mbunge mmoja anaweza kuibua hoja ya kuvunjwa kwa Katiba, ili Spika atoe uamuzi wa kurejesha majina ya wateule hao kwa Rais na kumshauri kuwa Katiba hampi mamlaka ya kuteua wanaume zaidi ya watano,” alisisitiza msomi huo mwenye Shahada ya Uzamivu.

Huku akielezea maana ya wabunge wasiozidi kumi, angalau watano kati yao wakiwa wanawake, alisema, “Rais angeweza  kuteua wanawake  wanane na wanaume wawili lakini si wanawake chini ya watano.”

Mhadhiri mwingine wa chuo hicho, Dk James Jesse alisema: “Inavyoonekana Rais hakutazama hicho kifungu, nadhani hilo ndio kosa lililofanyika. Hicho kifungu kiko sawa, kinasema angalau wanawake watano, maana yake wanawake wasipungue watano.”

“Kama ikiachwa hivi kutakuwa na uvunjifu wa Katiba, vinginevyo kama ikibainika hivyo ashauriwe vinginevyo, kama kuna ambao atawapunguza. Hapo ndipo inapotakiwa washauri wa Rais wafanye kazi kwa kutazama sheria kila wakati, lakini  wakijisahau  mambo kama haya hujitokeza.”

Serikali

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Profesa Sifuni Mchome alisema: “Huo ni mjadala uendelee tu. Katika mjadala watu hawazuiwi kujadili, binafsi sipo kwenye mjadala huo. Waache wajadili ufafanuzi kuhusu mjadala  hilo utatolewa wakati ukifika. Huwezi kuzuia watu kujadili.”

Chadema

Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alisema: “Hilo jambo mbona Katiba imeweka wazi. Sijui Spika atafanyaje siku ya kuapisha, maana uteuzi ni kinyume na Katiba. Tutaomba Mwongozo bungeni kuhusu suala hili, hatutanyamaza.”

Wakati Lissu akieleza hayo, Mwenyekiti wa Bavicha na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee alisema: “Tutakwenda mahakamani kupinga uteuzi huu, licha ya kujua kuwa Katiba iko wazi.

“Unapokuwa na neno ‘angalau’ tafsiri yake ni wasiwe chini ya watano, ila wanaweza kuwa zaidi ya hapo. Hadi sasa Rais ameteua robo tatu, hata hao waliobaki wawili, akiteua wanawake atakuwa amekiuka matakwa ya kikatiba, maana watakuwa hawafiki watano,” alisema Mdee.

Mdee alisema suala hilo si la wanawake wa Chadema pekee, linapaswa kupigiwa kelele na taasisi zingine kwa ajili ya kutetea wanawake.

Nani kunusurika?

Mapema baada ya uteuzi wa wabunge hao, wasomi na wataalamu wa siasa na utawala, walimzungumzia Profesa Kabudi kuwa uteuzi wake si wa kujaza viti vya ubunge pekee, bali umelenga kujaza moja ya viti kwenye Baraza la Mawaziri.

Mmoja wa wasomi hao, Dk Benson Bana wa UDSM alisema: “Siwezi kuwa mtabiri lakini ukisoma alama za nyakati na uteuzi huu kufanyika sasa, inawezekana si wote lakini nafikiri anaweza (Rais) kufanya mabadiliko kwenye Baraza la Mawaziri.

“Mfano Profesa Kabudi ni mzoefu, msomi na anaijua Tanzania. Ana uwezo mkubwa, wa kujieleza na kujenga hoja. Sidhani kama Rais atamwacha tu hivi hivi awe mbunge tu.”

Alisema Bulembo anaweza asiteuliwe kuwa waziri, lakini akatumika ndani ya Bunge kuimarisha umoja wa wabunge wa CCM.

Kikwete

Rais mstaafu Jakaya Kikwete katika muhula wake wa pili wa utawala, aliteua wabunge 10 na kati yao watano walikuwa wanawake.

Alimteua Zakhia Meghji na alipofanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri mwaka 2012, aliwateua Janet Mbene na Saada Mkuya na kuwateua kuwa naibu mawaziri Wizara ya Fedha.

Aidha, akamteua Dk Asha-Rose Migiro kuwa Waziri wa Katiba na Sheria na wakati anakaribia kuondoka madarakani, akamteua Dk Grace Puja.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo