Waume wanaonyanyaswa na wake waongezeka


Mery Kitosio, Arusha

IDADI ya wanaume wanaolalamika kuonewa na wenzao mkoani hapa imeongezeka kutoka walalamikaji 34 mwaka 2015 hadi kufikia 63 mwaka 2016 sawa na asilimia 48.

Akitoa taarifa hiyo ofisini kwake jana Mkuu wa Kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto wa Mkoa, Mkaguzi wa Polisi Happiness Temu alisema idadi hiyo imeongezeka hivyo kuonekana kuwa wanaume nao wanafanyiwa ukatili mkubwa na si wanawake peke yao.

Alisema ongezeko hilo lilitokana na kuenea kwa elimu inayotolewa na askari wa Dawati kwa watu wa jinsia zote kupitia vyombo vya habari hasa redio za hapa kwani hapo awali wanaume waliogopa kujitokeza kulalamika haswa wanapoonewa ndani ya ndoa zao.

Alifafanua kuwa wengi wa wanaume hao hufanyiwa ukatili wa kisaikolojia ambapo baadhi ya wenzao wanaonekana kutowathamini huku wengine wakikataa kushiriki tendo la ndoa, hali ambayo hufanya wanaume kujiona hawana uhalali wa kuishi na wenza wao.

“Mbali na ukatili wa kisaikolojia, pia baadhi yao hufanyiwa ukatili wa kiuchumi ambapo baadhi ya wanawake wenye uwezo kuzidi waume zao wakati mwingine hutoa uamuzi wa kifamilia pengine ukawa na maendeleo, lakini bila kushirikisha wenzi wao hali inayowafanya wabaini kwamba inatokana na kuzidiwa kipato na kushindwa kutengua uamuzi au kutoa ushauri,” alisema.

Alitaja wilaya inayoongoza kwa idadi ya wanaume kulalamika katika ofisi yake kuwa ni Arusha iliyokuwa na walalamikaji 48, Arumeru wanane na Ngorongoro watatu. Wilaya ya Longido ina wawili huku Karatu na Monduli zilikuwa mlalamikaji mmoja mmoja.

Alitoa mwito kwa viongozi wa kata, mitaa, vijiji na vitongoji kuiarifu ofisi yake wanapokuwa na vikao maeneo yao wazidi kusambaza elimu ya ukatili wa kijinsia kwa wanandoa, kwani wanaume wengi awali hawakuwa na ufahamu pia wanaweza kutoa malalamiko yao kupitia Dawati hilo.

Hata hivyo ofisi ya Dawati la Jinsia na Watoto mkoa wa Arusha mwishoni mwa mwaka jana imekuwa ikitoa elimu ya ukatili wa jinsia kwa wanafunzi wa shule za msingi zilizopo katika halmashauri ya Jiji la Arusha ambazo ni Sombetini, Osunyai, Ngarenaro, Kaloleni, Burka na Elerai hali ambayo imewasaidia wanafunzi hao kupata uelewa mkubwa juu ya ukatili.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo