Sababu za mawaziri wakuu kushindwa urais


Waandishi Wetu

Mwalimu Julius Nyerere
TANGU Tanzania ipate uhuru imekuwa na mawaziri wakuu 15, lakini miongoni mwao wapo waliojitosa kuwania urais bila mafanikio, huku wachambuzi wakitaja sababu 13 zinazofanya washindwe. Waziri Mkuu pekee aliyefanikiwa kuwa rais ni Julius Nyerere.

Miongoni mwa sababu za kushindwa mawaziri hao ambazo zilitolewa na wachambuzi ni pamoja na kitendo cha mawaziri hao kutetea hoja na mambo mbalimbali yanayofanywa na Serikali.

Kwa mujibu wa wachambuzi hao, kitendo hicho kinawafanya waonekane hawana jipya kwa kuwa mara nyingi Serikali inayomaliza muda wake huondoka na lawama nyingi.

Baadhi ya mawaziri wakuu waliojitosa kuwania urais na kuishia katika ngazi za awali ama mchujo ndani ya CCM ni Edward Lowassa ambaye jina lake likakatwa na Kamati Kuu na CCM na  baadaye akaamua kuhamia Chadema ambako aligombea kwa tiketi ya Chadema akiungwa mkono na Ukawa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Licha ya kushindwa, mara kadhaa Lowassa ameeleza  kuwa uchaguzi huo haukuwa wa haki na kubainisha kuwa atagombea tena mwaka 2020.

Wengine ni Salim Ahmed Salim, Mizengo Pinda, John Malecela, Frederick Sumaye na Cleopa Msuya.

Walichosema wasomi

Mhadhiri Mwandamizi wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana alisema sababu ya kwanza ni kusaka mgombea ambaye anajiuza kwa wananchi, bila kujali nafasi yake serikalini ndio sababu ya kukatwa kwa majina ya wagombea katika mchujo ndani ya CCM.

Alisema hiyo haina maana kuwa mawaziri hao walikuwa na makandokando, bali walizidiwa vigezo na wagombea wengine, hivyo majina yao kukatwa. Alisema vigezo vinavyotumika ni uwezo na uzoefu katika uongozi, uadilifu, unyenyekevu na busara.

Pia, elimu ya chuo kikuu au inayolingana na hiyo, mtu mwenye upeo mkubwa wa kuimarisha na kuendeleza Muungano, umoja na amani.

Alisema vigezo vingine ni kuwa mtetezi wa wanyonge na haki za binadamu na mtu asiye na  tamaa ya kujipatia umaarufu, kuzifahamu, kuzitetea na  kutekeleza sera na Ilani ya CCM, mpenda haki na ajuaye kupambana na dhuluma, kutokuwa mtu  mtu anayetumia nafasi ya uongozi kujilimbikizia mali.

Alisema kanuni za uteuzi wa wagombea katika Vyombo vya Dola, zinazoendelea kutumika ni zile zilizopitishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM ya mwaka 2010.

“Wananchi wanapenda mabadiliko ya uongozi, hivyo  tabia ya kujiibua badala ya kuibuliwa ni tatizo, Lowassa  hali hiyo itaendelea kumtesa hata 2020,” alisema.

Mwanasiasa mkongwe nchini, Nestory Kobelo alisema waziri mkuu ni mtendaji wa shughuli za kila siku za serikali, Rais anaposafiri nchi inakuwa chini yake.

Alisema rais anapokosea suala lolote la kiutendaji, waziri mkuu ndiyo aliyeshindwa kumshauri vizuri ili atekeleze wajibu wake wa kuwatumikia wananchi.

“Rais anapomaliza kipindi chake ya uongozi wa miaka 10 na  jina la waziri mkuu hubadilika na kuitwa mstaafu wa serikali iliyopita,”alisema.

Alisema uwajibikaji katika ngazi za chini kitatumika kama kigezo namba moja katika changuzi ndani ya CCM na siyo nafasi ya mtu.

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Abdulkarim Atiki alisema mfumo wa CCM hauzingatii nafasi ya mtu serikalini, hivyo hawawezi kumchangua mtu ambaye utendaji wake unafahamika.

Alisema CCM wanaogopa kuchagua waziri mkuu kwani kama kulikuwa na dosari katika utawala uliopita, wananchi watasema ni utawala uleule hakuna mabadiliko.

“Tanzania imejijengea sifa kwa kuibua marais kutoka ndani ya baraza la mawaziri tangu Awamu ya Pili hadi Awamu ya Tano,” alisema.

Mhadhiri mwingine wa UDSM Profesa Kitila Mkumbo alisema Msuya aliwahi kufikia tatu bora katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 1995.

“Unajua kinyang’anyiro hicho kilikuwa kikali baada ya Msuya kupenya, Rais mstaafu Benjamini Mkapa na Jakaya Kikwete na baadaye Mkapa akaibuka kidedea kuwa Rais,” alisema.

Historia ya mawaziri wakuu

Desemba 9, 1961 Nyerere alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Serikali ya Tanganyika kabla ya kujiuzulu na kumwamchia wadhifa huo, Rashid Kawawa ambaye aliteuliwa Januari 22, 1962 na kushika wadhifa huo hadi Desemba 1, 1962.

Kawawa aliteuliwa tena kushika wadhifa huo Februari 17,  1972 hadi Februari 13, 1977 na baada ya kung’atuka nafasi yake ilichukuliwa na Edward Sokoine.

Sokoine alishika nafasi hiyo ya mtendaji mkuu wa Serikali kuanzia mwaka 1977  hadi 1980 na kupokewa na  Msuya aliyedumu katika wadhifa huo kuanzia mwaka 1980 hadi 1983.

Mwaka huo huo, Sokoine alirejea tena na kudumu kwa takribani miezi 14 mpaka Aprili 12, 1984.

Wiki mbili baadaye, yaani Aprili 24, 1984, Dk Salim aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa tano na kudumu katika nafasi hiyo hadi Novemba, 1985.

Mwaka huohuo, Jaji Joseph Warioba aliteuliwa kushika wadhifa huo hadi mwaka 1990. Baada ya Jaji Warioba kung’atuka nafasi yake ilichukuliwa na John Malecela ambaye alikuwa Waziri Mkuu kuanzia mwaka 1990 hadi Desemba 7, 1994.

Msuya alirejea katika wadhifa huo Desemba, 1994 hadi Novemba 1995.

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, Frederick Sumaye aliteuliwa kushika wadhifa huo. Sumaye ndiye Waziri Mkuu pekee aliyedumu katika nafasi hiyo kwa miaka yote kumi.

Mwaka 2005 Lowassa aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu na kudumu  kwa miaka mitatu hadi Februari 7, 2008 alipojiuzulu kutokana na kashfa ya kampuni ya Kufua Umeme ya Richmond. Baada ya kung’atuka, nafasi yake ilichukuliwa na Mizengo Pinda mpaka mwaka 2015.

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Kassim Majaliwa aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu nafasi anayodumu nayo mpaka sasa.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo