Msajili wa Vyama aingizwa kwenye mapambano


Mwandishi Wetu

Jaji Mutungi (kulia)
SIKU chache baada ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Jaji Francis Mutungi kuidhinisha ruzuku ya CUF kwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba mikakati ya kumchafua imeanza chini kwa chini.

Mikakati hiyio inadaiwa kuratibiwa na Kamati ya Uongozi ya Chama hicho ambayo Msajili haitambui.

Taarifa ambazo gazeti hili limezipata zinadai kwamba mbinu hizo zimeanza kutekelezwa na viongozi wa Kamati hiyo kwa kusambaza habari zinazomdhalilisha Msajili wa katika vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii.

Moja ya mikakati hiyo ni iliyosambazwa na Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano, Mbarala Maharagande iliyojaa kejeli, matusi, tuhuma na dhihaka kwa Msajili na kuacha kujibu hoja za msingi ambazo awali zilitolewa na Ofisi ya Msajili.

Taarifa za ndani ya mkakati huo zinadai kuwa pamoja na mitandao ya kijamii, pia magazeti kadhaa likiwamo maarufu la kila wiki linalomilikiwa na wabunge wawili wa chama cha upinzani nchini yatatumika kufanikisha azma hiyo.

Maharagande alizungumza na waandishi wa habari huku akidai kuwa Ofisi ya Msajili inasababisha mpasuko ndani ya chama hicho na ndiyo maana imetoa ruzuku kwa Lipumba.

Aidha, JAMBOLEO ilizungumza na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro aliyesema Mutungi amevunja maadili ya kazi yake, hivyo hawawezi kumvumilia.

Alisema kwa sasa wanasheria wao wako kwenye mchakato wa kufungua kesi ili kushitaki wahusika wa wizi huo.

Akizungumzia taarifa hizo katika moja ya magazeti, Jaji Mutungi alisema haogopi kuchafuliwa vyovyote kwa kuzingatia ukweli kwamba yeye ni mtumishi wa umma na anafanya kazi zake kwa mujibu wa sheria za nchi na hawezi kuyumbishwa na matusi wala kejeli dhidi yake na ofisi yake.

"Na mimi nimezipata hizo taarifa, kwamba kuna baadhi ya watu wamepanga kupambana nami kwa kunichafua, japo naendelea kuzifanyia kazi, lakini kwa kifupi niwaambie waache wanichafue na wala siogopi lolote," alisema.

"Mimi ni mtumishi wa umma nafanya kazi kwa mujibu wa sharia, hivyo siwezi kuyumbishwa na mambo ya kitoto ya kuchafuana na kurushiana tuhuma zisizo na kichwa wala miguu. Sidhani kama kumshambulia Mutungi kunaweza kuleta tija ya wao kufikia malengo yao," alisema.

Aidha, alisema mjadala wa ruzuku ya CUF aliyoitoa kwa chama hicho ameshaufunga na anashangazwa na maneno ya uongo yanayozidi kusambazwa na watu wanaojiita viongozi wa CUF.

Jaji Mutungi alisema yeye ni muumini wa haki na sheria, na ndiyo maana mamlaka za uteuzi zilimwamini na kumpa ujaji.

"Natambua uadilifu wangu na sitaki niuelezee, ila nahisi tukiendelea kulizungumzia hili tutakuwa tunalikuza bila sababu za msingi.  Nasisitiza tena kuwa ofisi yangu inamtambua Profesa Lipumba kama Mwenyekiti wa CUF na Maalim Seif Sharif Hamad kama Katibu Mkuu,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, alisema kinachoendelea kufanywa na kundi la watu wanaojiita viongozi wa CUF ni kuzungumza mambo mengi ya uongo na kumhusisha bila ukweli huku wakishindwa kusoma vyema Katiba yao wenyewe.

"Nasisitiza tena si Mutungi au Ofisi ya Msajili iliyoandika Katiba ya CUF, ni wao wenyewe. Ofisi ilichofanya ni kuitafsiri na kutoa mwongozo. Sasa tatizo liko wapi?” Alihoji.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo