Waandishi waaswa kutumia takwimu sahihi


Suleiman Msuya

WAANDISHI wa habari nchini wametakiwa kutumia takwimu rasmi na kuzingatia kanuni katika kuandika taarifa za aina hiyo, ili kusaidia jamii.

Hayo yamesemwa na Mtakwimu Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Emillian Karugendo, wakati akiwasilisha mada kwenye semina elekezi kwa waandishi hao kuhusu Sheria ya Takwimu ya Mwaka 2015 na Sheria ya Makosa ya Mitandao iliyoandaliwa na Shirika la Kimataifa la Internews, Dar es Salaam.

Alisema kuzi kuwa iwapo waandishi watazingatia takwimu na kanuni katika mchakato   wa taarifa wanazotoa watasaidia jamii kupata elimu sahihi ya jambo husika.

Karugendo alisema msingi wa takwimu rasmi utaonesha mfumo mzima wa uzalishaji, uchakataji na usambazaji taarifa husika.

"Sisi NBS tunasimamia sheria na kanuni kuhakikisha misingi ya kuandaa takwimu inafuatwa na si kukandamiza mtu, hivyo taasisi na watu binafsi wanapaswa kutoa ushirikiano," alisema.

Mtakwimu huyo alisema baada ya sheria hiyo kupitishwa, wamepokea maombi   kutoka kwa watafiti ambao wanataka kukusanya takwimu.

Alisema sheria yoyote haiwezi kuwa rafiki kwa watu wote, hivyo kinachohitajika ni wadau kutoa mapendekezo katika kuhakikisha kila mdau anakuwa salama.

Karugendo alisema kwa sasa wanajikita kwenye utoaji elimu kwa wadau na jamii kwa ujumla jambo ambalo linaweza kutoa matokeo chanya ya sheria hiyo.

Mwanasheria wa NBS, Oscar Mangula alisema sheria hiyo imekuja kuiwezesha ofisi hiyo kuratibu mambo ya takwimu kwa uwazi zaidi.

Alisema kwa sasa wamo kwenye mchakato wa kukamilisha kanuni ili ziweze kufanya kazi pamoja na sheria.

Oscar alisema sheria hiyo inafanya kazi Tanzania Bara na Zanzibar hasa upande wa sensa ya watu.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo cha Takwimu, Dk Camilius Kasala alisema ili waandishi wa habari na watafiti waweze kushiriki kwa amani katika utekelezaji wa sheria ni muhimu kusoma Takwimu.

Alisema iwapo waandishi watafanikiwa kupata mafunzo ya takwimu, ni wazi kazi zitakwenda kwa uwiano sahihi.

"Pamoja na misingi mnayosimamia, mnapaswa kuepuka msukumo, upendeleo na msimamo katika kazi ambazo ni taarifa za takwimu," alisema.

Mwanasheria James Marenga alitoa mwito kwa waandishi kusoma sheria hiyo kwa makini kwa kuwa hawako salama.

Alisema sheria hiyo inagusa watu wengi hata ambao hawahusiki na takwimu.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo