Shibuda ataka wanasiasa kusoma alama za nyakati


Suleiman Msuya

John Shibuda
MWENYEKITI wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini, John Shibuda, amesema atatolea ufafanuzi kuhusu hatima ya mvutano ulipo kati ya vyama vya siasa na Serikali kuhusu mikutano ya hadhara ndani ya simu 21 zijazo.

Shibuda aliyasema hayo jana wakati akizungumza na vyombo vya habari, ikiwa ni takribani mwezi mmoja baada ya kuchaguliwa na baraza hilo kuwa mwenyekiti, akichukua nafasi iliachwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa APPT-Maendeleo, Peter Mziray.

Alisema tangu Serikali ya Awamu Tano iingie madarakani hali ya kisiasa imekuwa na mvutano mkubwa na hali hiyo imekuwa ikileta mivutano mikubwa.

Mwenyekiti huyo alisema ni jukumu la baraza kukaa na kutafari kuhusu mvutano huo uliopo alioeleza kuwa hauna tija kwa siasa za Tanzania.

Hata hivyo alieleza kuwa bado hakuna budi kwa vyama kuangalia njia sahihi ya kuwasiliana na Serikali na kuachana na tabia ya kutumia lugha zisizofaa ambazo zinasababisha kutofautina.

“Sisi kama Baraza tunahitaji vyama vya siasa na wanasiasa kufanya siasa za maendeleo na si za kulumbana, kwani hazina tija kwenye maslahi ya nchi,|” alisema.

Alivitaka vyama vya siasa kufikisha madai yao kwenye baraza hilo ili liweze kuchukua hatua stahiki na kuachana na utaratibu wa kila chama kuzungumza lake.

Shibuda alisema kauli za baadhi ya viongozi wa vyama vya kisiasa zinaweza kuwa sababu ya Serikali kufanya maamuzi ambayo yanalalamikiwa, hivyo kuwataka wasome alama za nyakati.

“Hakuna shaka kuwa mikutano ya kisiasa miaka ya nyuma ilichangia kutetereka kwa Serikali iliyopita, hivyo wanapaswa kutambua Serikali hii ni nyingine wanapaswa kusoma mazingira,” alisema.

Halikadhalika alisema pamoja na changamoto zilizopo za kisiasa nchini, bado uhuru kwa vyama vya siasa unahitajika ili kuhakikisha haki za kisiasa zinatekelezwa.

Shibuda alitumia mkutano huo kumpongeza Rais John Magufuli kwa kile alichodai kuwa amefanikiwa kurejesha heshima ya utumishi, kudhibiti mianya ya rushwa, ubadhirifu na wizi katika Serikali.

Aidha, alimpongeza Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuiongoza nchi hiyo kwa kufuata misingi ya utawala bora na kuwataka wananchi kumuunga mkono.

Alisema ni jukumu la wananchi kuwaunga mkono ikiwa ni kwa kufanya kazi ambazo zitaongeza pato lao na kukuza uchumi wa nchi na kuondoa matabaka ambayo yamekuwepo kwa muda mrefu.

Katika mkutano huo ulikuwa na wajumbe wa vyama vya siasa vicahche huku vyama vya upinzani vyenye wabunge vikiwa havina wawakilishi.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo