Walemavu waipongeza Serikali kuwasikiliza


Peter Akaro

Ummy Nderiananga
SHIRIKISHO la Vyama vya Walemavu Tanzania (Shivyawata), limeipongeza Serikali kwa kusikia kilio chao juu ya vifaa tiba, ila limebainisha kuwa suala la usafiri bado changamoto kwao.

Mwaka jana shirikisho hilo lililalamikia kauli ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu aliyebainisha kuwa kundi hilo linapaswa kujigharamia vifaa tiba na matibabu.

Lakini mwenyekiti wa Shivyawata, Ummy Nderiananga, alisema jana kuwa baadaye Waziri Mwalimu alisikia kilio chao na akatoa agizo kwa hospitali kuendelea kuhudumia watu wenye ulemavu.

“Pia tuliomba bima ya afya kwa walemavu na Serikali ilishaanza mchakato wa kutupatia na vitu vingine tulivyoomba ni kama mafuta ya albino na walishatupatia kwa hiyo mambo yanaendekea vizuri,” alisema.

Nderiananga alisema huduma hizo kwa kiasi kikubwa zimefika mikoani na wao kama viongozi hawajapata shida au mamalalamiko kutoka huko.

Kuhusu usafiri kwa walemavu ndani Maradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (Udart), Nderiananga alisema bado kuna changamoto.

Alitaja changamoto hiyo kuwa ni kukosekana kwa nafasi ya kukaa watu wenye ulemavu ingawa kwenye mabasi hayo kuna viti vilivotengwa kwa ajili ya makundi maalumu kama wazee na wajawazito na walemavu.

Alisema suala hilo wanajaribu kulishughulikia na pia kwenda mbali zaidi kwa kuangalia kama walemavu wanaweza kusafiri kwa gharama nafuu au bure kabisa kwa sababu mradi huo ni wa Serikali.

“Hili linazungumzika na tumepanga kwenda huko kupata utatuzi wa hii changamoto,” alisema Nderiananga.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo