Warioba alia hali ya chakula nchini


*Asema dalilili zilizopo zisichukuliwe kisiasa
*Aasa wanasiasa wakabiliane nayo pamoja

Mwandishi Wetu

Jaji Joseph Warioba
WAZIRI Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, amesema zipo kila dalili ya nchi kukumbwa na upungufu wa chakula, hivyo wanasiasa bila kujali itikadi zao, wanapaswa kuungana kubuni mikakati na hatua za kuchukua kudhibiti hali hiyo.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mwenyekiti huyo wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba alisema si sahihi kuendelea kubishana kuwa nchi ina njaa au haina, wakati dalili zinaonesha uwezekano wa kukumbwa na upungufu wa chakula.

“Watanzania tuwe pamoja kulikabili hili kama tulivyokuwa tukifanya huko nyuma. Hili ni suala la kitaifa, ni lazima tuungane kujua wakati huu tunafanya nini na hali ikiharibika tufanye nini, tusilifanye suala hili kuwa la kisiasa,” alionya Jaji Warioba.

Alisema nchi kukumbwa na upungufu wa chakula ni jambo la kawaida na si jipya, kwa vile limekuwa likitokea miaka ya nyuma kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo mvua kutonyesha kwa wakati.

Huku akieleza jinsi Rais wa Awamu ya Kwanza, Julius Nyerere alivyokuwa akihimiza wananchi kulima na kuhifadhi chakula ikitokea nchi inakumbwa na upungufu wa chakula, alitaja mambo manne yanayopaswa kufanyika ili kukabiliana na kadhia hiyo.

Sakata la nchi kukumbwa na njaa liliibuka katika maeneo mbalimbali huku vyombo vya habari vikiripoti taarifa za wananchi kushindia maembe na mifugo kufa, kutokana na ukame.

Wanasiasa na wasomi walizungumzia jambo hilo na kuitaka Serikali kuchukua hatua za haraka huku viongozi wa dini wakienda mbali zaidi na kuwataka waumini wao wafanye hija, mfungo, mikesha na maombi ili kunusuru hali hiyo.

Jumatatu wiki hii, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema Serikali itagawa tani milioni 1.5 za chakula zilizobaki msimu uliopita katika maeneo yenye uhitaji mkubwa ili kupunguza kasi ya ongezeko la bei za vyakula nchini, lakini akakana taarifa kuwa nchi ina njaa.

Wakati Majaliwa akitoa ufafanuzi huo, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba, alisema Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), katika mwaka wa fedha wa 2016/17 imepanga kununua tani 100,000 za chakula, na hadi Januari 8, wakala huyo alikuwa amenunua tani 62,087 za mahindi.

Lakini jana, Jaji Warioba alisema licha ya nchi kujitosheleza kwa chakula kuna baadhi ya maeneo yana upungufu unaosababisha utegemezi wa chakula kutoka sehemu zingine za nchi.

“Ndiyo maana tumekuwa na mikoa ambayo inasikifika kwa uzalishaji chakula. Lakini mwaka huu kwa dalili hizi na mambo yanayoambatana na mabadiliko ya tabianchi, inaonekana kutakuwa na upungufu wa chakula kwa sehemu kubwa,” alisema.

Aliongeza, “hii inatokana na mvua kutonyesha kama inavyotarajiwa. Hili si jambo jipya limewahi kutokea miaka ya nyuma.”

Alisema kwa kuwa kuna dalili za upungufu wa chakula ni lazima kujiandaa kukabiliana na hali hiyo, ikiwamo kuhadharisha wananchi.

“Pia lazima kusaidia wananchi kutumia njia zitakazowawezesha kupata mazao. Hilo linapaswa kufanywa na Serikali na watu wa kada mbalimbali. Hapa wananchi wanaweza kupewa elimu au mbegu zinazostahimili ukame,” alisema.

Alisema, “bado tuna muda maana kuna sehemu ambazo zinapata mvua za vuli. Licha ya mvua kutonyesha kama ilivyozoeleka, wananchi washauriwe kuzitumia vizuri, ni wajibu wa Serikali kusaidia wananchi hata kama wanahitaji mbegu.”

Kwa mujibu wa Jaji Warioba, nchi inapokumbwa na upungufu wa chakula, wananchi pia wanapaswa ama kulima au kuhifadhi chakula na si kusubiri Serikali ishughulikie suala hilo.

“Nakumbuka mwaka fulani nchi ilikumbwa na upungufu wa chakula, Serikali iliwataka wananchi walime. Nakumbuka Nyerere aliwaeleza wananchi walime, la sivyo tutakufa na watu walilima kila mahali,” alisema na kuongeza:

“Wenye uwezo wanunue chakula na kukitunza. Haifai tuanze kulumbana, maana mwisho wa siku Serikali itajitahidi kuziba pengo la upungufu kama upo,” alisema.  

Aliongeza kuwa viongozi bila kujali vyama, jambo la kwanza wanalopaswa kufanya ni kuhimiza wananchi watumie mvua zinazonyesha sasa kupanda mazao, pili, kutathmini hali ilivyo na kama itatokea waamue watafanya nini.

Alisema si sahihi kuendelea kubishana kuwa nchi ina njaa au haina njaa, wakati dalili zinaonesha uwezekano wa kukumbwa na upungufu wa chakula.

“Watanzania tuwe pamoja kulikabili hili, kama tulivyokuwa tukifanya huko nyuma. Hili ni suala la kitaifa hivyo ni lazima tuungane,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo