Obama aombwa aingilie kati


*Wamkumbuka siku chache baada ya kuondoka Ikulu
*Kiini ni matamko na uamuzi wa kila siku ya Rais mpya

CALIFORNIA, Marekani

Donald Trump
CHINI ya siku 10 za urais wa Trump inaonekana kwamba kila siku kunaibuka vita vipya na baadhi ya Wamarekani wanamtaka Rais mstaafu Barack Obama aingilie kati.

“Vita dhidi ya ukweli. Vita dhidi ya urais wa Mexico. Vita dhidi ya vyombo vya habari. Vita dhidi ya mazingira. Vita dhidi ya NATO (Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Ulaya). Vita dhidi ya Waislamu.

“Vita dhidi ya Mfumo wetu wa Uchaguzi. Vita dhidi ya nyota wa Hollywood. Vita dhidi ya haki za wanawake. Vita dhidi ya China. Vita dhidi ya miiko ya Rais. Vita dhidi ya wakimbizi.” Anaandika Maclen Zilber, Mwana Mikakati na Mshauri wa Masuala ya Kampeni wa Democrats aliyeko Hollywood, California

Urais wa Obama una siku chache tu nje ya Ikulu, na tayari maswali yameanza kuibuka juu ya kama vita hivi alivyovichochea Trump vitakwisha.

Msimamo wa Rais huyu wa sasa wa kuendelea ‘kumwaga petroli kwenye moto’ huku akionesha uhasama wa wazi wazi duniani, nyumbani na kimataifa, unazidi kusababisha mvutano ndani na nje ya Marekani, wakati akipanda mbegu ya mgogoro, vurugu na ghasia kwenye sayari hii.

Kwa kuelewa kabisa, Rais Obama aliweka wazi kwamba atamfanyia wema Donald Trump kama ilivyofanywa na viongozi waliomtangulia, atakaa kimya na kumruhusu Rais mpya aongoze nchi bila kuingiliwa na mtangulizi wake, anasema Zilber.

Lakini kutokana na umaarufu alionao kwa Wamarekani na watu wengine nje ya Taifa hili, hivi sasa ni muda mwafaka kwa Rais Obama kuvunja taratibu na ukimya wake.

Kwa sasa, katika kipindi hiki cha kiza, tunahitaji msemaji wetu mkuu wa Taifa letu, afute vumbi viatu vyake na arejee uwanjani. Mtu ambaye alishawishi Taifa kuamini kwamba sisi si majimbo mekundu wala bluu. Kijana mwembamba mwenye jina la kuvutia, ambaye kuna wakati alitufanya tuamini katika matumaini na mabadiliko.

Kitu pekee kinachoweza kushinda hofu ni matumaini. Rais Obama, tunajua umetoa kila kitu ulichokuwanacho kwa ajili yetu, na hatuna haki yoyote ya kukutaka kujitolea maisha yako zaidi. Lakini Wamarekani wanahitaji talanta zako, tunahitaji sauti yako, tunahitaji kalamu yako ya unyoya, na tunahitaji uadilifu wako.

Ulisema mara ya mwisho, kwamba ungeweza kumshinda Donald Trump kama ungeshindana naye moja kwa moja. Ni muda sasa wa kuthibitisha hilo.

Vitendo vya Trump vinaibua maswali zaidi juu ya kama hatua zake hatari na za ubaguzi zinawaweka Wamarekani na binadamu wote wa Dunia hii, kwenye mwelekeo wa mgongano ambao unaweza kusababisha vita vya dunia.

Kwenye kiini ambacho kinaufanya urais wa Trump kuwa wa hatari zaidi ni nia yake ya wazi ya kuwaona Wamarekani kama watu wanaoweza kudanganyika kirahisi.

Mara ya kwanza Trump alifanya hivyo kupitia kwa Msemaji wa Ikulu, Sean Spicer, kuhusu umati uliohudhuria kuapishwa kwake. Akafanya hivyo tena kesho yake alipokwenda makao makuu ya Idara ya Ujasusi (CIA), akieneza upotoshaji kama alivyofanya Spicer.

Katika tukio hilo hilo, Trump alipotosha ukweli juu ya uhusiano wake na taasisi hiyo ya intelijensia, akisema vyombo vya habari vilitengeneza uzushi kwamba ana uhusiano mbaya na chombo hicho, ambapo siku chache kabla ya kuapishwa kwake alikifananisha na “Ujerumani ya Wanazi,”

Siku iliyofuata, na siku ya tatu ya urais wake, mshauri wake mwandamizi, Kellyanne Conway alikataa kukanusha uongo wa Trump, na badala yake akauita “ukweli mbadala,” kwenye kipindi cha NBC cha Meet the Press (Kutana na Waandishi).

Mbaya zaidi, siku ya nne, baada ya kuapishwa kuwa amirijeshi mkuu wa 45 wa Marekani, Trump aliwadanganya viongozi wa Bunge la Congress, akisema kulikuwa na udanganyifu mkubwa wa upigaji kura kiasi cha kura hewa kati ya milioni 3 na 5 kwenye uchaguzi wa Novemba 16.

Madai hayo ya uongo kimsingi yalishusha uhalali wa uchaguzi wake kama Rais wa Marekani, lakini pia mfumo mzima unaounganisha pamoja demokrasia yetu ya uwakilishi.

Uongo huu umejikita zaidi kwenye nini kinachotarajiwa kutokea katika miaka kadhaa ijayo ya utawala wa Trump na kwa bahati mbaya, tabia yake ya udikteta, ukichaa na ukurupukaji, imeongeza kuuweka hatarini usalama wa kila Mmarekani.

Fikiria. Kama Trump anapenda kuendelea na uongozi wake usio na msingi juu ya uchaguzi wake mwenyewe, baada ya madai yake ya kuwapo udanganyifu kupingwa au   idadi ya watu waliohudhuruia sherehe zake za kuapishwa kutokana na hisia zake za kutaka kuonekana bora zaidi pamoja na udhaifu alionao, ni nini kitamzuia kudanganya juu ya mgogoro wa kidunia utakaoliweka Taifa letu kwenye sintofahamu?

Hatua kama hiyo itasababisha vita, umwagaji damu na hata upotevu wa maisha ya Wamarekani – na hatutaweza hata kujua kama anaweza kuamini visingizio vinavyosemwa kuhusu vita hivyo.

Zaidi ya uongo wake usio na soni, nguvu zake nyepesi za kalamu azitumiazo kusaini maagizo ya utendaji au maandiko yake kwenye mitandao ya kijamii, ya kibaguzi kwa viongozi wengine wa dunia, zinasababisha sintofahamu na mabadiliko makubwa duniani - na havionekani kumshitua au hata washauri wake hata kidogo.

Mambo yote haya yanaonekana kuubainisha ukweli, kwamba kila siku inayopita, ukosefu wa utulivu unachemka chini kwa chini duniani na maumivu yanazidi kuongezeka ndani ya Marekani yakiongozwa na kiongozi wetu mfitini, Donald Trump.

Ulisema mara ya mwisho, kwamba ungeweza kumshinda Donald Trump kama ungeshindana naye moja kwa moja. Ni muda sasa wa kuthibitisha hilo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo