Shinikizo la damu chanzo cha kifafa cha mimba


Salha Mohamed

DAKTARI bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Tarimo Vecent ametaja shinikizo la damu la juu kwamba linasababisha kifafa cha mimba, huku Mkoa wa Pwani ukiongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi.

Ugonjwa huo unaokuwa kwa kasi katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, umetajwa kusababishwa na mfumo wa maisha na msongo wa mawazo, huku maskini wakiathirika zaidi.

Dk. Vecent alisema kifafa cha mimba huanza wiki ya 20 ya ujauzito ambapo miongoni mwa dalili zake ni kuumwa kichwa, presha kuwa juu, kutokuona vema, maumivu kwenye chembe.

“Wakati mwingine si lazima shinikizo kuwa kubwa, lakini kinachosababisha ni kupungua kichwani kwa usambazaji wa hewa ya oksijeni ndipo anapata kifafa,”alisema.

Alisema shinikizo la damu husababisha mishipa ya damu kusinyaa na kusababisha mzunguko wa damu kuwa mdogo na kupungua zaidi na hapo ndipo kifafa kinapotokea.

Dk. Vicent anafafanua kuwa kifafa cha mimba hakirithiwi huku akibainisha mimba za kwanza ndiyo hupata zaidi.

“Ugonjwa huu mara nyingi huwa tunazuia zaidi kuliko tiba kwani kila mjamzito anapopata kifafa husababisha hitilafu kichwani hivyo matibabu huanzia kwenye kuzuia kwa kuanza kliniki mapema,” alisema.

Alisema wagonjwa wanaofikishwa hospitalini hapo wakiwa na hali mbaya ambapo huwapa dawa aina ya Sulphatehuku akibainisha kila mjamzito anayepata kifafa kuna kiasi cha ubongo huathirika na kupata upungufu mwilini.

Alisema kifafa ni moja ya madhara ya Shinikizo la damu ambapo mjamzito anaweza kupata kiharusi, kutokuona kwasababu ya mishipa ya damu kupasuka, matatizo ya ini, matatizo ya figo.

“Shinikizo la damu husababisha viungo vya mwili kufa kama ini,figo, kichwani huathirika yote sababu ya shinikizo la damu kutokufuatiliwa vema tangu mwanzo,”alisema.

Alisema wanawake wengi wanaofikishwa hospitalini hapo wanakuwa hawajitambui huku wengine wakiwa wanajitupa huku na kule ambapo hupoteza fahamu.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Wagonjwa wa Kifafa cha Mimba hospitalini hapo, Alice Msondo kuzaa na wanaume tofauti, umri mkubwa, magonjwa ya shinikizo la damu, kisukari na figo ni miongoni mwa viashiria vya kifafa cha mimba.

“Hali duni ya maisha husababisha watu kupata kifafa cha mimba sababu ya msongo wa mawazo, na hwapata masikini wengi zaidi kuliko matajiri.

“Wagonjwa wengi tuliokuwa nao hapa ni masikini mtu anakuja kujifungua hana hata kanga na ni wagonjwa wa msamaha,”alisema.

Alisema katika hospitali hiyo hupata wagonjwa 80 hadi 120 kwa mwezi huku idadi hiyo ikionekana kuongezeka katika miaka mitatu.

“Tatizo linakuwa hasa miaka mitatu hii, kutokana na hali ya maisha msongo wa mawazo na hata hali ya hewa kama ambavyo Pwani huathirika zaidi,”alisema.

Alisema ugonjwa huo hauchaugui umri kwani hupata wenye umri wa miaka 16, mimba za kwanza na hata wenye umri mkubwa.

Alisema wanawake wengi wanaopata ugonjwa huo hupoteza watoto au kupata mtoto njiti ambapo hospitali huakikisha anajifungua ndani ya saa 8 ili kuokoa maisha ya mama.

Aliitaka jamii kutambua muhimu wa kuwahi kliniki, kutambua muda wa kubeba mimba ili kuepuka msongo wa mawazo na kupata madhara kwani ni ugonjwa wa pili kusababisha vifo vya mama na mtoto nchini.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo