Baraza la Mawaziri kutikiswa


*Ni kutokana na uteuzi wa wabunge Kabudi, Bulembo
*Kila mteule wa ubunge JPM amekuwa akimpa uwaziri

Fidelis Butahe

Rais John Magufuli
KUNA kila dalili kwamba uamuzi wa Rais John Magufuli kuwateua Profesa Palamagamba Kabudi na Abdallah Bulembo kuwa wabunge, ni ishara ya kufanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri.

Hatua hiyo inatajwa kuchagizwa na taaluma na uzoefu wa wateule hao na utendaji wa mawaziri takribani mwaka mmoja tangu kuteuliwa kushika nyadhifa hizo.

Uchunguzi wa JAMBO LEO na maoni ya wachambuzi wa masuala ya siasa nchini unabainisha, kwamba Rais Magufuli kimfumo na matukio yanayoendelea nchini, yakiwemo yanayozikumba wizara, huenda akafanya mabadiliko hayo ili kuendeleza kasi yake ya ‘Hapa Kazi Tu’.

Uteuzi wa Kabudi ambaye ni Profesa wa Sheria wa Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Bulembo ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, umefanya idadi ya wabunge walioteuliwa na Rais Magufuli kufikia wanane, huku watano wakiteuliwa kuwa mawaziri, mwingine Dk Tulia Ackson kuwa Naibu Spika wa Bunge.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema: “Siwezi kuwa mtabiri, lakini ukisoma alama za nyakati na uteuzi huu kufanyika sasa, inawezekana si wote, lakini nafikiri anaweza (Rais Magufuli) kufanya mabadiliko katika Baraza lake.

“Mfano Profesa Kabudi ni mzoefu, msomi na anaijua Tanzania. Ana uwezo mkubwa, wa kujieleza na kujenga hoja. Sidhani kama Rais atamwacha hivi hivi awe mbunge tu.”

Alisema Bulembo anaweza asiteuliwe kuwa waziri, lakini akatumika bungeni kuimarisha umoja wa wabunge wa CCM.

“Huenda Magufuli anataka umoja wa CCM usimamiwe vizuri. Binafsi naamini bado Lowassa (Edward) ana ushawishi miongoni mwa wabunge wa CCM wa sasa. Bila kutafuta mbinu za kuhakikisha mizizi yake inakatwa taratibu, italeta shida. Wanaangalia mwaka 2020 maana yeye (Lowassa) ameanza kampeni mapema,” alisema Dk Bana.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inampa Rais mamlaka ya kuteua wabunge wasiozidi 10 kutoka miongoni mwa wananchi ambao anaona wanaweza kumsaidia katika utekelezaji wa majukumu yake kwenye baadhi ya maeneo kama vile afya, elimu, kilimo, nishati na sheria.

Ibara ya 66 (1) inasema, bila ya kuathiri masharti mengine ya ibara hii, kutakuwa na aina zifuatazo za wabunge, yaani (e) wabunge wasiozidi 10 walioteuliwa na Rais kutoka miongoni mwa watu wenye sifa kwa mujibu wa ibara ya 67, isipokuwa sifa iliyotajwa katika ibara ya 67 (1) (b).

Walioteuliwa

Miongoni mwa wateule hao ni Naibu Spika, Dk Tulia. Novemba mwaka juzi Naibu Mwanasheria Mkuu huyo wa zamani alichukua fomu za kuwania uspika kupitia CCM kabla ya kujitoa dakika za lala salama, na akateuliwa na Rais Magufuli kuwa Mbunge wa Viti Maalumu.

Baada ya kujitoa, alijitosa kuwania unaibu spika ambapo wabunge 250 walimpigia kura ya ndiyo.

Wengine walioteuliwa kuwa wabunge na kupewa wizara ni, Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Augustino Mahiga, Profesa Makame Mbarawa (Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano), Profesa Joyce Ndalichako (Elimu), Dk Philip Mpango (Fedha) na Dk Abdallah Posi  Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu.

Rais Magufuli alipoteua Baraza la Mawaziri Desemba 10 mwaka juzi, walikuwamo Dk Posi, Balozi Mahiga na Profesa Mbarawa ambao waliteuliwa kwanza kuwa wabunge.

Wakati akitangaza Baraza hilo, alisema aliacha viporo wizara nne za Maliasili na Utalii, Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Fedha na Mipango na Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, huku akiteua naibu mawaziri kuongoza wizara hizo.

Desemba 23 alimalizia kiporo hicho kwa kumteua Profesa Ndalichako na Dk Mpango kuwa mawaziri ikiwa ni baada ya kuwateua kuwa wabunge.

Akizungumzia uteuzi huo, mhadhiri mwingine wa UDSM, Richard Mbunda alitofautiana na Dk Bana na kusisitiza: “Kwa kuzingatia utendaji wa mawaziri wenyewe na hali ilivyo sasa, sidhani kama kuna sehemu (wizara) imelega. Unajua Magufuli wakati akiteua mawaziri alizingatia sana weledi.

“Ndiyo maana Dk Mwakyembe (Harrison) yuko Wizara ya Katiba na Sheria, hata Mahiga amebobea katika masuala ya uhusiano wa kimataifa na yuko Wizara ya Mambo ya Nje. Huyu Makamba (Januari-Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais- Mazingira na Muungano), Shahada yake ya Uzamili amesomea masuala ya utatuzi wa migogoro.”

Alisisitiza kuwa iwapo wizara kadhaa zingekuwa zimetetereka, huenda uteuzi wa Profesa Kabudi ungeashiria kuwa anakwenda kuziba pengo katika maeneo hayo.

“Nadhani anajaribu kuongeza idadi ya wabunge bungeni maana nafasi 10 za uteuzi wa Rais huongeza nguvu ya CCM bungeni. Sioni kama kuna kitu chochote kimemsukuma kufanya uteuzi huu,” alisema Mbunda.

Rais Magufuli tangu alipotangaza kuunda wizara 18 zenye mawaziri 19 na manaibu 16, huku sita kati yao wakiwa wanawake, amefanya mabadiliko kwa kutengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga na kumteua Mwigulu Nchemba aliyekuwa Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo kushika wadhifa huo.

Kupitia mabadiliko hayo, Rais alimteua Dk Charles Tizeba kuziba nafasi ya Mwigulu.

Katika mwaka mmoja wa utawala wake, Rais Magufuli alimtosa waziri mmoja, kuhamisha mmoja na kuteua mmoja wakati mtangulizi wake, Jakaya Kikwete alihamisha mawaziri 18.

Kikwete

Katika muhula wa pili wa utawala wake, Rais Kikwete aliteua wabunge 10, kati yao sita aliwapa wizara za kuongoza, utaratibu ambao Rais Magufuli aliutumia ili kupata mawaziri kulingana na mahitaji ya Serikali yake.

Walioteuliwa na Kikwete kuwa wabunge na kupewa wizara, ni Profesa Mbarawa, Shamsi Vuai Nahodha, Zakhia Meghji, Profesa Sospeter Muhongo, Janet Mbene, Saada Mkuya na Asha-Rose Migiro. Alikamuilisha orodha yake ya uteuzi wa wabunge 10 kwa kuwateua Dk Grace Puja na Innocent Sebba ambao hakuwapa uwaziri.

Kabudi

Profesa Kabudi ambaye alipata kuwa Mkuu wa Kitivo cha Sheria UDSM, alihitimu Shahada ya Sheria UDSM akipata daraja la kwanza mwaka 1983 na Shahada ya Uzamili mwaka 1986 katika chuo hicho.

Alisoma Shahada ya Uzamivu ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Freie kilichoko Berlin, Ujerumani mwaka 1995. Profesa huyo pia ni Msajili wa Kanisa la Anglikana Tanzania na pia alikuwa mjumbe wa Iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Bulembo

Bulembo ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM tangu mwaka 2012, pia alipata kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Soka cha Mkoa wa Mara (MRFA) na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Kwenye Kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka juzi, alikuwa Meneja wa Kampeni wa Mgombea Urais wa CCM.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo