Mawaziri mguu ndani mguu nje


Waandishi Wetu

Baraza la Mawaziri
RAIS John Magufuli anatarajia kuipanga safu yake ya Baraza la Mawaziri wakati wowote, huku baadhi ya naibu mawaziri na wabunge aliowateua wakipewa nafasi kubwa ya kuteuliwa kuwa mawaziri.

Hatua hiyo inatokana na uamuzi wake wa kumteua aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Dk Abdallah Posi kuwa balozi na hivyo kufanya nafasi hiyo kubaki wazi.

Historia inaonyesha kuwa Rais Magufuli  amekuwa na utaratibu wa kuwapa uwaziri wabunge ambao amewateua.

Ukiacha Posi ambaye aliteuliwa kuwa mbunge na kisha waziri, wabunge wengine walioteuliwa na kiongozi mkuu huyo wa nchi na kuteuliwa kuwa mawaziri ni;  Profesa Joyce Ndalichako (Elimu), Dk Agustino Mahiga (Mambo ya Nje), Profesa Makame Mbarawa (Ujenzi, Uchukuzi na Mwasiliano) na Dk Philip Mpango (Fedha)  huku Dk Tulia Ackson ambaye naye aliteuliwa kuwa mbunge, akichaguliwa kuwa Naibu Spika.

Wiki iliyopita Rais Magufuli aliteua wabunge wawili, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Abdallah Bulembo na nguli wa sheria, Profesa  Paramagamba Kabudi.

Kutokana na utaratibu huo na uzoefu wa wateule hao, wachambuzi waliozungumza na gazeti hili walisema huenda Profesa Kabudi na Kilango wakateuliwa kuwa mawaziri.

Katika orodha hiyo, Kilango ambaye alikuwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga  ametajwa kutokana na kuwa miongoni mwa wateule saba wa Rais, ambao kati yao sita wamepewa wizara.

Wachambuzi hao wamesema pia nafasi ya Posi inaweza kuzibwa na mbunge  mlemavu kwa maelezo kuwa historia inaonesha kuwa akiondolewa waziri kutoka ukanda fulani, atateuliwa wa kutoka ukanda huo huo, iwapo aliyeondolewa alikuwa mlemavu, basi atarejeshwa mlemavu.

Kauli za wasomi

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino, Profesa Mwesiga Baregu alisema, “Rais Magufuli si mtu anayetabirika kwa sababu hakuna aliyeamini kuwa atamrejesha Kilango bungeni na kumteua Posi kuwa balozi. Kuna uwezekano mkubwa nafasi ya Posi ikajazwa na Profesa Kabudi maana ni mwanasheria pia.”

“Ingawa Kabudi ana nafasi lakini huwezi kuwapuuza wabunge wengine. Huenda Magufuli akateua miongoni mwao kuziba nafasi ya Posi.”

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Benson Bana alisema litakuwa jambo jema iwapo Rais Magufuli atamteua mlemavu kuziba nafasi ya Posi, huku akimtaja mbunge wa viti maalum (CCM), Amina Mollel.

 “Ikiwa atafanya hivyo itakuwa vizuri zaidi. Binafsi naona mabadiliko makubwa katika baraza la mawaziri. Naona wazi uwepo wa Profesa Kabudi katika baraza la mawaziri maana ni hazina ya taifa amejaliwa kipaji cha kufikiri cha hali ya juu,” alisema.

Vigezo uwaziri

Ikiwa Rais Magufuli ataendeleza utaratibu wa mtangulizi wake wa kuteua waziri kutoka mkoa anaotoka waziri aliyeondoka, wabunge kutoka mikoa ambayo mawaziri wataoondolewa, wataula katika uteuzi huo.

Nani kubaki?

Wakati ikisubiriwa mabadiliko hayo wapo baadhi walikuwa mawaziri katika Serikali iliyopita, kufanikiwa kuteuliwa tena katika Serikali ya Awamu ya Tano.

Mawaziri hao ni Profesa Jumanne Maghembe, Profesa Sospeter Muhongo, William Lukuvi, Dk Hussein Mwinyi, Profesa Mbarawa, Dk Tizeba, Gerson Lwenge, Charles Mwijage, Jenister Mhagama, Mwigulu Nchemba, Ummy Mwalimu, Angela Kairuki, January Makamba, George Simbachawene na Dk Harrison Mwakyembe.

Miongoni mwao, Dk Mwinyi amefanikiwa kuwemo  ndani ya baraza la mawaziri bila kutoka nje ya uwanja.

Mwaka 2005 alichaguliwa kuwa waziri aliyeshughulikia masuala ya Muungano, mwaka 2008 alipewa kuongoza Wizara ya Ulinzi na mwaka 2012 aliteuliwa kuiongoza Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

Mwingine ni Profesa Jumanne Maghembe, mwaka 2006 aliteuliwa kuwa Waziri wa Kazi, nafasi aliyoishika kwa miaka miwili hadi mwaka 2008 alipokabidhiwa mikoba ya kuiongoza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Mwaka 2010 alipewa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Maji anayoiongoza hadi hivi sasa.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo