Balozi Sefue aingia jopo la watu mashuhuri


Mwandishi Wetu

Balozi Ombeni Sefue
ALIYEKUWA Katibu Mkuu Kiongozi na Mwanadiplomasia, Balozi Ombeni Sefue, ameteuliwa kuwa Mtanzania wa kwanza kuingia katika Jopo la Watu Mashuhuri katika Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM).

Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa APRM, tawi la Tanzania Rehema Twalib anayehudhuria Mkutano wa Umoja wa Afrika (AU) unaendelea mjini Addis Ababa nchini Ethiopia, Balozi Sefue aliidhinishwa na kikao cha juu cha viongozi wa umoja huo.

Alisema nafasi hiyo ya kuwa katika jopo la APRM haikuwa rahisi kutokana na nchi nyingi kuwasilisha majina ya watu mashuhuri.

“Balozi Sefue amefanikiwa kuingia katika jopo hilo la watu mashuhuri, ila naamini inaweza kuchangiwa na utumishi uliotukuka na kuungwa mkono na Serikali ya Awamu ya Tano,” alisema.

Twalib alisema APRM ni mpango wa Afrika uliobuniwa na wakuu wa nchi kwa lengo la kuwa na chombo kitakachosaidia kuhimiza nchi wanachama kuenzi utawala bora na utoaji wa huduma bora za kiuchumi, kibiashara na za kijamii kwa wananchi wao kupitia mfumo wa kujitathmini zenyewe na kukosoana.

Katibu Mtendaji huyo alisema kuwa APRM ni chombo cha juu cha kuwashauri wakuu wa AU katika uendeshaji wa mpango huo na hususani mchakato mzima wa kujitathmini.

Alisema wajumbe hao wa APRM wanahitajika kudumu kwa muda wa miaka minne hiyo ikiwa ni baada ya mchakato mrefu kufanyika ikiwa ni pamoja na ushindani wa wahusika.

Katibu huyo alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi 35 wanachama wa UA kati ya nchi 54 zilizojiunga na APRM. Ilijiunga mwaka 2004 na kwa sasa inaendelea kuteleleza mapendekezo ya mpango huo.

Twalib aliwataja wajumbe wengine walioteuliwa kuwa ni Profesa Ibrahim Gambari kutoka Nigeria, Balozi Mona Attia Misri, Fatma Kadaria Algeria, Askofu Don Sengulane Msumbiji na Profesa Augustin Loada Burkina Faso.

Aidha, alisema wajumbe wa zamani wanaondelea ni Profesa Youssouf Khalal (Chad), ambaye atakuwa mwenyekiti wa jopo na Brigitte Mabandla Afrika Kusini ambaye ni Makamu Mwenyekiti.

Alisema pamoja na kuchaguliwa kwa wajumbe hao pia mkutano huo ulijadili ripoti za tathmini za nchi katika maeneo ya anuai ya utawala bora kwa nchi za Kenya, Sudani, Chad, Senegali, Djibouti na Zambia.

Mwenyekiti wa AU ambaye pia ni Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta aliwapongeza wajumbe hao na kuwataka kushiriki vyema katika kuihuisha APRM na kuwa chombo chenye thamani kubwa kwa Afrika kama walivyotarajia waasisi wake.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo