Mawaziri wakuu wastaafu wafunguka


Suleiman Msuya

Jaji Joseph Warioba
MAWAZI wakuu waliopata kuingia kwenye kinyang’anyiro cha urais kupitia CCM, wamesema siri ya wao kukosa nafasi hiyo ni demokrasia, haki, uwazi na utawala bora kwenye mchakato.

Kauli hizo za mawaziri wakuu zinakuja siku moja baada ya wachambuzi kubainisha sababu 13 za wagombea wenye sifa ya uwaziri mkuu kushindwa kupenya kwenye kinyang’anyiro hicho ndani ya CCM.

Baadhi ya sababu za wachambuzi hao ni mawaziri wakuu hao kutetea hoja za Serikali zilizopita, kusaka mgombea anayejiuza kwa wananchi, elimu, mtetezi wa wanyonge na haki za binadamu, asiye na tamaa na mwajibikaji.

Warioba

Akizungumzia sababu ya yeye kukosa nafasi hiyo ya katika chama chake, Jaji Joseph Warioba alisema anaamini demokrasia inapewa nafasi zaidi.

Warioba alikwenda mbali na kusema CCM inazingatia misingi ya usawa, haki na kuepuka ubaguzi, hivyo kila anayegombea huangaliwa kwa haki sawa.

“Wakati tunachukua fomu hakuna anayeangaliwa kwa cheo kuwa wewe ni waziri mkuu, hiyo haipo wote tuko sawa,” alisema.

Alisema ili kuhakikisha taasisi au chama kinakuwa imara ni lazima taratibu zifuatwe, hivyo hajaona kosa kwa wao kuachwa na kupitishwa anayehitajika au kufaa zaidi yao.

Msuya

Cleopa Msuya alisema wakati wa uchaguzi kinachofanyika ni timu moja ambayo inakuwa na mitazamo tofauti, lakini pale ambapo mmoja wao anachaguliwa hakuna tatizo.

Msuya alisema kinachohitajika ni demokrasia kupewa nafasi yake na kuachana na dhana kuwa kuna upungufu au upendeleo.

“Kwa mimi naamini kinachofanyika ni demokrasia kupewa nafasi zaidi nadhani tuendelee kujenga nchi kwa kuwapa ushirikiano wanaopewa nafasi ya kuongoza,” alisema.

Sumaye

Fredrick Sumaye ambaye kwa sasa ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alisema pamoja na kuwapo dhana ya demokrasia, mchakato huo ndani ya CCM unaingiliwa na ubinafsi, hasa kwa rais anayemaliza muda wake kutaka mtu anayehisi atamlinda.

Sumaye alisema pia ipo dhana kwa wajumbe hujenga imani kuwa waziri mkuu amekuwa mtendaji, hivyo kumwona kama hajulikani kwani kazi zake nyingi ni za kiutendaji zaidi.

Aidha, alisema mfumo wa upitishaji wagombea ndani ya CCM ni sababu nyingine ambayo inawakwamisha, kutokana na Mwenyekiti kuja na jina lake hasa akichagua mtu asiye maarufu kuliko yeye.

“Pia kuna sababu ya watu kufikiria kuwa nafasi ya urais ni ya ulaji jambo ambalo si kweli, hivyo kusababisha vita kwenye mchakato,” alisema.

Historia inaonesha nchini aliyefanikiwa kutoka uwaziri mkuu na kugombea urais akashinda ni Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere pekee, huku Warioba, Msuya, Sumaye, Edward Lowassa, Mizengo Pinda, Dk Salim Ahmed Salim na John Malecela wakijaribu bila mafanikio.

Hali hiyo ilianza kuibua maswali kwa wananchi wakitaka kujua siri  imejificha kwa viongozi hao kukosa kupitishwa urais.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo