Wastaafu EAC wamwomba Magufuli awaokoe


Charles James

Rais John Magufuli
WASTAAFU wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ya zamani wamemwomba Rais John Magufuli kuingilia kati malalamiko yao ya madai ya pensheni ambayo wamekuwa wakiidai Serikali tangu kuvunjika kwa Jumuiya hiyo Juni 30, 1977.

Mkataba wa kuvunjika kwa Jumuiya hiyo uliosainiwa mwaka 1984 na marais wa Jumuiya hiyo, Julius Nyerere wa Tanzania, Milton Obote wa Uganda na Daniel arap Moi wa Kenya, uliagiza kulipwa kwa wastaafu hao na watumishi waliokuwa wamesitishiwa ajira zao.

Akizungumza kwenye mahojiano maalumu na JAMBO LEO, Mwenyekiti wa wastaafu hao, Mohamed Ngunde ambaye alikuwa mtumishi wa Shirika la Posta na Simu, alisema kwa kipindi kirefu wamefuatilia malipo yao Hazina, lakini hakuna hatua ambayo imechukuliwa zaidi ya kuendelea kupigwa danadana.

Alisema wamekuwa wakifuatilia mafao yao katika awamu zote za uongozi ambapo Novemba 11, 1991 aliyekuwa Makamu wa Rais na Waziri Mkuu, John Malecela aliwaandikia barua kuwataka kuacha kusumbuka, kwani hakuna wanachodai na hawatalipwa.

Ngunde alisema barua ya Malecela iliwashangaza, lakini waliendelea kudai haki yao na mwaka 1999, walionana na aliyekuwa Waziri wa Fedha wakati Jumuiya hiyo ikivunjika, Cleopa Msuya ambaye alikiri kuwa Serikali ilipaswa kuwalipa kama mkataba wa kuvunjika kwa Jumuiya hiyo ulivyoagiza.

“Baada ya kuonana na Msuya Serikali ilianza kutulipa, ingawa malipo hayakuwa ya kuridhisha kwani wapo watumishi waliotoka mikoani lakini waliishia kulipwa Sh 10, Sh 30 hadi Sh 150.

“Mwaka 2003 tulifungua kesi ya kudai mafao yetu, lakini Serikali ikamwomba Jaji Kimaro aliyekuwa Mahakama Kuu kufuta kesi hiyo ili wakafanye suluhu, jambo ambalo kwa mujibu wa Mkataba halikuwa sahihi, kwani hakukutakiwa mazungumzo tena zaidi ya kulipwa stahiki zao,” alisema Ngunde.

Katika hotuba yake Mei mosi, 2005 Rais Benjamin Mkapa alikiri kufahamu Mkataba huo na kuahidi kuwalipa wastaafu hao zaidi ya Sh bilioni 400 ingawa kidogo kidogo.

“Kila mmoja anajua namna gani nimekuwa nikiheshimu wazee, hivyo nawaahidi kuwa nitahakikisha kabla sijaondoka madarakani watumishi wote wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanaodai mafao yao wanalipwa,” ilisema sehemu ya hotuba ya Mkapa.

Katibu wa Wastaafu hao, Hamad Wenge ambaye ni mrithi kutokana na baba yake kutumikia Shirika la Reli, alimwomba Rais Magufuli kuingilia kati madai yao, ili walipwe kama wenzao wa Kenya na Uganda.

Alisema baada ya tamko la Mkapa walianza kulipwa ingawa walipewa Sh milioni 2 pekee ambazo zilikuwa za nauli na kibaya zaidi watumishi waliolipwa walikuwa ni 31,444 badala ya 17,500 waliokuwa halali.

“Tunamwomba Rais Magufuli aingilie kati, kwani tumekuwa tukimwandikia barua atusaidie au akutane nasi, lakini zimekuwa hazijibiwi jambo ambalo linaonesha kwamba wasaidizi wake hawamfikishii na mara ya mwisho tulimwandikia Aprili 4 mwaka jana.

“Tunajua Rais amekuwa akijali maslahi ya masikini na hata kwenye barua zetu tulirejea kauli zake wakati wa kampeni ambapo aliahidi kama angeshinda angehakikisha masikini wanaishi kama malaika,” alisema Wenge.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo