Bodi ya Mikopo yaendelea kuchambua majina


Hussein Ndubikile

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini (HESLB) imesema inaendelea na uchambuzi wa majina yaliyowasilishwa na waajiri ili kubaini waajiriwa wanufaika wanaotakiwa kurejesha fedha za mikopo.

Hatua hiyo imekuja baada ya Bodi hiyo kufanya msako wa ofisi kwa ofisi katika kampuni za Dar es Salaam na kuagiza waajiri wote kuwasilisha majina ya waajiriwa iweze kubaini wanaokwepa kurejesha.

Akizungumza na gazeti hili juzi, Meneja Urejeshaji Mikopo wa Bodi hiyo, Deodatus Mwiliko alisema baada ya msako huo na kuagiza waajiri walete majina ya waajiriwa wao kwenye ofisi za HESLB walitekeleza na kinachofanyika sasa ni uchambuzi wa kina kubaini wanufaika.

“Tunaendelea na uchambuzi wa majina ya wanufaika yaliyoletwa na waajiri tukishamaliza kuchambua tutawakata makato kama sheria za Bodi zinavyoelekeza,” alisema.

Alisema Bodi ilikagua kampuni 24 na kubaini kasoro zikiwamo za kutowasilisha majina ya waajiriwa, kuwasilisha makato pungufu nje ya muda na waajiri kutofahamu sheria za Bodi.

Alizitaja baadhi ya kampuni hizo kuwa ni shirika la ndege la Precison Air, Pepsi, Jambo Plastics, Jumbo Plastics, Sadolin na Tanzania Printers Ltd.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo, Abdul-Razaq Badru wanufaika walio kwenye ajira rasmi wanatakiwa kukatwa asilimia 15 ya mishahara yao na ambao hawako kwenye ajira isiyo rasmi watakatwa asilimia 10 ya kipato wanachopata kwa mwezi.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo