Trump aanza na Waislamu, ukuta


*Azuia wahamiaji kutoka mataifa ya Kiislamu
*Asisitiza kuanzaujenzi wa ukuta wa Mexico

WASHINGTON, DC, Marekani

Donald Trump
RAIS Donald Trump ameanza kuchukua hatua za kiutendaji kuhusu uhamiaji, akianza na kuimarisha ulinzi mpakani – ikiwa ni pamoja na kutekeleza mapendekezo yake ya ujenzi wa ukuta kwenye mpaka wa Marekani na Mexico.

Rais pia atachukua hatua katika siku chache zijazo za kupiga marufuku kwa muda uhamiaji wa watu kutoka nchi za Kiislamu zenye viashiria vya ‘tishio la usalama kwa taifa’ – ambazo ni Syria, Iran, Iraki, Libya, Yemen, Sudan na Somalia.

Halikadhalika, Trump amejipanga kusaini hatua zingine za ndani kuhusu kuimarisha masuala ya uhamiaji ikiwa ni pamoja na kulenga majiji ambayo ni kimbilio la wengi, lakini yanashindwa kuwashitaki wahamiaji wasio na nyaraka muhimu. 

Hata hivyo, taarifa zilisema pamoja na jana kuidhinisha kuanza kwa ujenzi wa ukuta huo, masuala mengine ya uhamiaji ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku watu kutoka nchi za Kiislamu kuingia Marekani, yataanza kutekelezwa baadaye wiki hii.

Juzi Rais alituma ujumbe kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter akielezea juu ya matamko mazito aliyopanga kuyatoa jana: “Kesho ni siku kubwa kwa usalama wa Taifa …miongoni mwa mambo mengine, tutajenga ukuta huo!”

Maelekezo hayo mapya ya Trump pia yatazuia wakimbizi wengi kuingia nchini wakiwamo wa kutoka Syria wakati michakato ya mchujo ikifanyika.

Tofauti pekee ni waumini wachache wanaokimbia ghasia – ambayo itahusu Wakristo wanaokimbia Syria na nchi zingine zenye Waislamu wengi, kwa mujibu wa wasaidizi wengi wa Bunge na wataalamu wa uhamiaji walioelezwa kuhusu suala hilo.

Mipango iliyopendekezwa ni pamoja na kusimamishwa kwa takriban miezi minne kwa ruhusa ya wakimbizi kuingia nchini, lakini pia marufuku ya muda mfupi ya wahamiaji kuingia nchini kutoka nchi zenye Waislamu wengi, kwa mujibu wa wawakilishi wa shirika la sera ya umma ambalo linafuatilia masuala ya wakimbizi.

Pia kutakuwa na utofauti katika kuzuia wakimbizi ambao wanakimbia unyanyasaji wa kidini, hasa kama dini yao ina watu wachache ndani ya nchi husika. Hiyo itahusu Wakristo wanaokimbia nchi zenye Waislamu wengi.

Rais huyu anayetoka chama cha Republican alitarajiwa jana kusaini amri hizo jijini hapa kwenye Wizara ya Usalama wa Ndani, ambayo majukumu yake ni pamoja na uhamiaji na usalama wa mipaka.

Akiwa kwenye kampeni, Trump alipendekeza kuwekwa marufuku ya muda dhidi ya Waislamu wanaoingia nchini, lengo likiwa ni kulinda Wamarekani dhidi ya mashambulizi ya kijihadi.

Trump na Mwanasheria Mkuu mteule, Seneta Jeff Sessions walishasema watajielekeza katika kubana nchi ambazo wahamiaji wao wanaweza kuwa tishio, kuliko kupiga marufuku watu wa dini fulani.

Wafuasi wengi wa Trump walishutumu uamuzi wa Rais wa Democratic, Barack Obama wa kuongeza idadi ya wakimbizi wa Syria waliosajiliwa nchini, kwa hofu kwamba waliokimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo, wanaweza wakatekeleza mashambulizi ya kigaidi nchini.

Wapinzani wa sera za Trump wanaweza kufungua pingamizi la kisheria kama nchi zote zinatazoguswa na marufuku hiyo ni zenye Waislamu wengi, alisema mtaalamu wa masuala ya uhamiaji, Hiroshi Motomura wa Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Los Angeles. Hoja za kisheria zitaweza kudai kwamba amri hizo zinabagua dini fulani, hatua ambayo ni kinyume cha Katiba, alisema.

“Kauli zake wakati wa kampeni na baadhi ya watu kwenye timu yake, zililenga zaidi dini kama lengo mahsusi,” Motomura alisema.

Stephen Legomsky ambaye alikuwa mshauri mkuu kwenye Huduma za Uraia na Uhamiaji nchini wakati wa utawala wa Obama, alisema Rais ana mamlaka ya kudhibiti uingiaji wakimbizi nchini na utoaji viza kwa nchi mahsusi kama utawala utaona kwamba ni kwa maslahi ya umma.

“Kwa mtazamo wa kisheria, hiyo itakuwa ndani ya haki zake za kisheria,” alisema Legomsky profesa katika Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Washington kilichoko St. Louis. “Lakini kwa mtazamo wa kisera, litakuwa ni wazo la kushangaza, kwa sababu kuna haki ya mahitaji ya kibinadamu kwa wakimbizi.”

Ili kuzuia watu kutoka nchi hizo kuingia nchini, Trump anaweza kuagiza Wizara ya Mambo ya Nje kuacha kutoa viza kwa watu wa mataifa hayo, kwa mujibu wa vyanzo vinavyohusika na mchakato wa utoaji viza.

Anaweza pia akaagiza wanaohusika na Ulinzi wa Forodha na Mipaka ya Marekani kuzuia wenye viza tayari wanaotoka nchi hizo kuingia nchini.

Msemaji wa Ikulu ya White House, Sean Spicer alisema juzi, kwamba Wizara za Mambo ya Nje na Usalama wa Ndani, ndizo zitashughulikia mchakato wa uchuchaji  mara tu mteule atakayeongoza Wizara ya Mambo ya Nje, Rex Tillerson atakaposimikwa rasmi.

Hatua zingine zitajumuisha maelekezo kwa mashirika yote kukamilisha kazi kwenye mfumo wa utambuzi wa wasio raia wanaoingia au kuondoka nchini, na kuendesha msako dhidi ya  wahamiaji wanaohudumiwa na serikali bila halali, kwa mujibu wa wasaidizi wa Bunge na wataalamu wa uhamiaji.

Akiwa rais, Trump anaweza pia akaagiza kusimamishwa kwa michakato yote ya kupokea wakimbizi. Rais George W. Bush alitumia madaraka hayo mara baada ya shambulizi la kigaidi la Septemba 11.

Msisitizo wa Trump kwamba Mexico ndiyo itakayogharimia ujenzi wa ukuta ni miongoni mwa mapendekezo maarufu yaliyotawala kampeni zake ambayo kila mara yalipokewa kwa shangwe kwenye mikutano yake. Hata hivyo, Mexico mara kwa mara imesisitiza kuwa haitagharimia chochote.

Maoni

Akizungumzia uamuzi huo wa Trump, Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum amesema anachokifanya Trump ni mwendelezo wa kujenga uadui na chuki kwa  Waislamu huku akisisitiza kuwa kitendo hicho kitafanya waumini wa dini duniani wamchukie yeye na Marekani.

“Huu ni mwendelezo wa chuki kwa Waislamu, matendo ya kigaidi hayafanywi na Waislamu jina la mtu haliwakilishi tabia yake, akumbuke kuwa Waislamu hawapo kwenye mataifa hayo bali wako dunia nzima,” alisema.

Alisema suala hilo litamletea shida kwenye utawala wake hasa kiuhusiano na mataifa mengine na hata raia wake watachukiwa na Ulimwengu.

Aliyekuwa Mjumbe wa Bunge la Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu alisema Trump amefanya uamuzi huo bila kuangalia matokeo ya baadaye kwa Taifa hilo huku akiongeza kuwa suala hilo linaweza kuleta vurugu na hali mbaya kiuchumi.

Alisisitiza kuwa kuna raia wanaotoka mataifa hayo wanaojishughulisha na biashara, hivyo hutumia usafiri wa anga na maji kuingia nchi hiyo, hivyo agizo hilo litasababisha biashara kuwa ngumu.

“Trump ameamua kabla ya kujua matokeo yake yatakuwa nini, ni jambo litakaloleta vurugu kwenye usafiri wa anga na maji, si wote wanaoingia Marekani ni wakimbizi bali wanaishi kwa shughuli za kibiashara,” alisema Mwesiga.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Helen Kijo-Bisimba alisema anachofanya Trump si sahihi, kwani mtu hawezi kuzuiwa kuingia nchi nyingine kwa kuangalia  dini yake huku akiongeza kuwa kufanya hivyo ni kinyume na Sheria za Mikataba ya Kimataifa ya Haki za Binadamu.

Alisema Marekani ikianza kutekeleza sheria hiyo, itakwenda kinyume na matakwa ya Shirika la Haki za Binadamu Duniani, ingawa Taifa hilo lina utaratibu na sheria zake.

Mjumbe wa Wainjilisti wa Kikristo Tanzania (UWAKITA), Elieza Shinza alisema jambo aliloamua kiongozi huyo ni sahihi, kwa kuwa mataifa hayo yana ajenda ya kueneza Uislamu duniani kwa njia yoyote ile, hivyo hata hilo lisipojitokeza leo linaweza kujitokeza miaka 20 ijayo.

“Mtazamo wetu tunajiuliza kwa watu hawa wakimbilie Marekani wasiende mataifa mengine ndipo tukagundua kuwapo mpango mkakati wa kueneza Uislamu,” alisisitiza.

Pia alisema inavyoonekana jinsi wanavyozidi kuongezeka wanaweza kuanza kufunga ndoa na kuzaliana, hali inayotishia huenda baadaye wakaja kuwa viongozi ndani ya Taifa hilo.

 *Imeandikwa na Hussein Ndubikile na mitandao






Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo