Kauli ya Masauni kuhusu njaa yatatiza


Abraham Ntambara

Hamad Yusuf Masauni
WATU mbali mabali wamelaani kauli ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni aliyoitoa juzi akiwa Rukwa akiagiza Jeshi la Polisi kukamata wanasiasa watakaotangaza kuwapo njaa nchini.

Hivi karibuni, Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) liliandika barua kwa maaskofu wa makanisa yote nchini kuliombea Taifa ili mvua inyeshe kwa kuwa kipindi hiki kilikuwa kinatarajiwa kuwa na mvua lakini hali imekuwa tofauti.

Ilifuatiwa na taarifa ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) nalo likiwataka maimamu na mashehe misikitini kuongoza Waislamu kuliombea Taifa lipate mvua na kuondoa ukame na baa la njaa linalolinyemelea.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na JAMBO LEO jana Dar es Salaam, watu hao walisema kauli hiyo haina mantiki, hivyo kumtaka ahimize Polisi itimize wajibu wake wa kulinda usalama wa raia na mali zao, kwa kuwa agizo lake linakiuka Katiba inayompa mtu uhuru wa kutoa mawazo.

Mbunge wa zamani wa Kigoma Kusini, David Kafulila alisema kauli ya Naibu Waziri kuzuia watu kuzungumzia njaa na kuagiza watakaokiuka wakamatwe ni kinyume na Katiba, inazuia uhuru wa kutoa maoni.

Kafulila alisema kauli hiyo haina tija na Jeshi la Polisi lina shughuli nyingi za kufanya kuliko agizo hilo, hivyo ingekuwa busara kama angelihimiza kuhakikisha linalinda usalama wa raia.

“Hata Rais alipokataza watu kuzungumzia njaa, TEC na Bakwata walisisitiza msimamo wa kuwapo dalili za njaa,” alisema Kafulila.

Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema aliilaani agizo hilo kwa maelezo kuwa ni kauli  isiyo ya kitanzania.

“Haiwezekani watu wana njaa wakae kimya kwa sababu wanaogopa kukamatwa,” alisema Mrema.

Aidha, alisema ilitakiwa waanze kukamata viongozi wa dini waliotangaza kuliombea mvua Taifa, ambapo alibainisha kuwa tangu enzi za Mwalimu Julius Nyerere hatukuwahi kuwa na viongozi wenye kauli za namna hiyo wasiotaka wananchi kusema ukweli wa hali halisi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa CUF, Julius Mtatiro alisema kauli hiyo haina maana yoyote kwa sababu si vibaya kusema kuwa sehemu fulani kuna njaa.

“Kama atasubiri Rais atangaze kuwapo njaa, yeye aendelee kumsubiri, Rais atatangaza wakati yeye anakula,” Alihoji Mtatiro.

Alisema vijijini kuna njaa na hali inazidi kuwa mbaya ambapo alieleza kuwa kama kauli yake itakuwa hivyo, afungue magereza ya kuwaweka kwa kuwa hawataacha kusema kuna njaa nchini.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maadili, Amani na Haki za Jamii kwa Madhehebu ya Dini nchini, Askofu William Mwamalanga alisema kauli hiyo imekosa weledi, kwa kuwa hakuna anayependa njaa akieleza kwamba Rais alikwishasema hakuna njaa.

“Rais anaposema hakuna njaa ina maana kwamba hata ikiwapo yuko tayari kushughulikia,” alisema Askofu Mwamalanga.

Alisema kauli hiyo ni ya kutaka kumfurahisha Rais ambapo alibainisha kuwa hiyo si kazi yake kwa kuwa Mkuu wa Nchi alikwishasema na badala yake alitakiwa kuliagiza Jeshi la Polisi kusimamia usalama wa raia na si vinginevyo.

Masauni

Hata hivyo, Masauni alifafanua kuwa kauli yake ilitokana na taarifa ya mkoa wa Rukwa kuonesha kuwa eneo hilo halina njaa, hivyo akaonya kuwa hatarajii kusikia watu watakaojitokeza kusema kuna uhaba wa chakula mkoani humo.

Isitoshe alisema taarifa ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Zelothe Steven ilionesha kuwa mkoa una chakula cha ziada, lakini kuna baadhi ya wanasiasa wanaodai kuwapo njaa mkoani humo.

“Kauli ya Mkuu wa Mkoa ni sawa na ya Rais katika eneo hilo. Sitarajii mwanasiasa au mtu yeyote kutoa taarifa kwamba mkoa wa Rukwa unakabiliwa na njaa.  Ikitokea hivyo, utakuwa ni uchochezi hivyo mhusika kustahili kuchukuliwa hatua,” alisema Masauni. 
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo