Mwenyekiti CCM apigwa risasi


Moses Ng’wat, Mbeya

MWENYEKITI wa CCM wa Wilaya ya Mbeya, Ephaim Mwaitenda, amejeruhiwa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.

Mwaitenda ambaye kwa sasa amelazwa katika hospitali ya Rufaa Mbeya akiendelea na matibabu, alipigwa risasi mgongoni akiwa amelala usiku wa manane wa kuamkia jana kibandani shambani mwake, Kyela.

Akithibitisha tukio hilo jana, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Emmanuel Lukula alisema tukio hilo lilitokea juzi saa nane usiku shambani kwake.

Hata hivyo, Kaimu Kamanda Lukula alisema hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa ingawa taarifa za awali zinaonesha kuwa huenda tukio hilo lilifanywa na watu wa karibu na Mwenyekiti huyo.

Akifafanua alisema kabla ya watu hao kumjeruhi Mwenyekiti kwa risasi walitoboa dirisha kwa kukata nyavu na kuingiza mtutu na kumfyatulia risasi mgongoni.

“Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa bunduki iliyotumika kwenye shambulio hilo ni ya kienyeji kwani risasi zilizotumika ni golori na kama ingekuwa ni bunduki ya kisasa asingenusurika,” alifafanua Kamanda Lukula.

Hata hivyo, Kamanda alisema baada ya watu hao kutekeleza tukio hilo, walikimbilia kusikojulikana bila kuchukua kitu chochote.

“Jitihada za kuwakamata waliohusika zinaendelea kwa kuwa askari Polisi waliofika eneo la tukio walipata baadhi ya vitu muhimu katika uchunguzi vinavyodhaniwa kudondoshwa na watu waliotekeleza tukio hilo,” alisema Kamanda.

Katibu wa CCM wa Mkoa wa Mbeya, Zongo Lobe Zongo alisema hali ya Mwenyekiti huyo inaendelea vizuri kutokana na jitihada za madaktari wa Hospitali ya Mbeya kumfanyia uchunguzi wa awali, ikiwamo kumtoa risasi mwilini.

“Kama utakuwa mvumilivu naomba unipigie baada ya muda kwani hivi sasa tuko hapa X-ray (Chumba cha Mionzi) madaktari wanampiga picha ili wakamtoe risasi, lakini hali yake si mbaya, kwani nimeongea naye,” alisema.

Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, Dk Godlove Mbwanji akizungumzia hali ya majeruhi baada ya kupokewa hospitalini hapo, alisema hali yake inaendelea vizuri na alipelekwa chumba cha upasuaji kutolewa risasi.

“Alikuja hapa akiwa na hali nzuri kwani anazungumza na tulipomfanyia vipimo vya awali kama presha ilikuwa sawa na baadaye mchakato wa kumfanyia uchunguzi wa jeraha lake mgongoni ambalo linaonekana kama limetobolewa na bisibisi na kwa mtazamo ni risasi za mtawanyiko,” alifafanua Dk Mbwanji.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo