Wanawake hawanufaiki na jasho lao – Utafiti


Salha Mohamed

WANAWAKE wanamiliki asilimia tisa tu ya ardhi au mashamba nchini, ingawa kundi hilo ndilo linalozalisha chakula kwa asilimia 60, ikilinganishwa na wanaume.

Hayo yalibainisha Dar es Salaam jana wakati wa mkutano wa waandishi wa habari kuhusu Mradi wa Uhamasishaji wa Usawa wa Kijinsia katika Kilimo, uhakika wa Chakula na Lishe kutoka Shirika la Land O’Lakes.

Mshauri Mwelekezi wa Usawa wa Kijinsia  wa shirika hilo, Magreth Henjewele alisema tafiti zinaonesha kuwa kilimo ni nguzo ya taifa kwa kuwa maendeleo ya uchumi yanakitegemea.

“Kwa mujibu wa utafiti uliofanyika mwaka jana inaonesha kilimo ndiyo kinaongoza kwa kuchangia asilimia 29 katika pato la taifa ukilinganisha na sekta nyingine,”alisema.

Alisema wanawake ndiyo wenye mchango mkubwa katika kilimo, lakini humiliki ardhi kwa asilimia ndogo ambapo katika utafiti wa masuala ya kazi wa mwaka 2014 unaonesha wanawake huchagia zaidi ya asilimia 51 ya nguvu kazi katika kilimo.

Magreth alisema katika uzalishaji mazao ya kilimo wanawake wamekuwa wakishiriki zaidi, huku wakiwa hawanufaiki na kile walichokizalisha.

Alisema jamii inatakiwa kuelimika katika masuala ya kijinsia katika kilimo na mgao wa manufaa kutokana na uzalishaji wa mazoa ya kilimo.

Mkurugenzi wa Shirika hilo, Dk Rose Kingamkono alisema mbali na kilimo kuwa uti wa mgono lakini kinatoa ajira takribani asilimia 70 hapa nchini.

“Bahati mbaya sekta ya kilimo imegubikwa na nyenzo ambazo ni duni, na kusababisha uzalishaji wake kutokuwa mzuri huku nguvu kazi kubwa wakiwa ni wanawake,”alisema.

Alisema kutokana na nyenzo duni wamekuwa wakitumia muda mwingi katika uzalishaji na kuathiri afya zao pamoja na watoto waliopo tumboni kwa wajawazito.

Alisema hadi sasa tayari wametoa semina 25 katika kaya 7000 katika mikoa wa Morogoro, Iringa, Dodoma kwa wananchi ili kujua usawa wa kijinsia katika kilimo kama upatikanaji wa ardhi, kufanya kilimo biashara na hata kujua sheria zilivyo.

Aidha mtafiti na mchambuzi wa sera na masuala ya kijinsia, Profesa Bertha Koku alisema amegundua kuwa katika sera za hapa nchini zinamaeneo ya uwezeshaji na kumsaidia mwanamke kujikomboa na kujiimarisha katika uchumi, kimaisha, kisiasaa kupata haki zake na rasilimali.

“Katika sera hizo tumegundua kuwa kuna maeneo ambayo ni kandamizi hivyo tunaendeleza pale ambapo tunaona mwanamke anaweza kunufaika na kilimo na kunufaika na jasho lake,”alisema.

Alisema juhudi zichukuliwe na taasisi zingine katika kuhakikisha wananchi wanaelewa hasa katika kujiendeleza katika kilimo kwa wanawake na hata kusaidiana kazi ngazi ya familia.

Alisema kuna umuhimu wa kutangaza sera na watu wazifahamu ili wazitumie katika kudai haki zao kwani hawazifahamu na kushindwa kuzitekeleza.

“Sera kwa kiasi kikubwa ni nzuri lakini utekelezaji ndiyo unakuwa na matatizo sana basi tujaribu kuona mikakati gani inatumika ili watu wazifahamu na kuzitekeleza,”alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo