Mpinga ashitukia matrafiki waonevu


*Ni wanaobambika kesi kwa madereva, aomba taarifa
*Adaka mmoja, amtoza faini aliyomwandikia ‘mkosaji’

Stella Kessy

Mohammed Mpinga
KAMANDA wa Kikosi cha Usalama barabarani, Mohammed Mpinga, ametaka wananchi wanaotozwa faini za makosa barabarani kinyume na makosa husika, kuwasilisha malalamiko yao kwake, ili askari waliofanya kitendo hicho wachukuliwe hatua.

Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Dar es Salaam jana, Mpinga alisema jambo hilo halikubaliki na kusisitiza kuwa kila anayefanya kosa anapaswa kutozwa faini kulingana na kosa husika, si kulazimisha alipe faini hata kama hajafanya kosa, huku gari lake likiwa halina tatizo.

Ufafanuzi wa Kamanda Mpinga umekuja takribani siku tatu, baada ya mkazi wa Dar es Salaam, kukamatwa na askari akidaiwa kuweka kioo cha giza kwenye gari, lakini alipofikishwa kituoni ikabainika kuwa aliweka kipande kidogo kwenye kioo cha mbele ili kuzuia mwanga wa jua.

“Unajua, tumezuia wenye magari kuweka vioo vya giza, hasa kioo cha mbele na pembeni. Huyu aliyekamatwa alikuwa ameweka robo tu kioo cha mbele kwa ajili ya kuzuia mwanga wa jua,” alisema Mpinga huku akionesha picha ya gari hilo.

Baadaye Kamanda huyo akaandika kwenye mtandao wa kijamii na kusisitiza: “Nilimwita yule askari na kumweleza kuwa alichokifanya si sahihi na kumtaka ailipe faini aliyoiandika.”

Hivi karibuni kumeibuka mvutano mkali kati ya askari wa usalama barabarani na baadhi ya madereva wanaokamatwa kwa makosa mbalimbali, huku wengi wakilalamika kuonewa kwa kubambikiwa makosa.

“Iko tabia ya baadhi ya watu kulazimisha kuandikiwa kosa na baadaye kulalamika. Madereva wengi wakiona wametendwa jambo ambalo hawajaridhika nalo, hawapendi kuona viongozi wakati namba zetu zipo,” alisisitiza Kamanda Mpinga.

Mbali na kufafanua kuhusu jambo hilo, Kamanda Mpinga alisema mchakato wa kubadili faini za makosa ya usalama barabarani unaendelea, lengo ni kuongeza kutoka 30,000/- za sasa.

Alisema uamuzi huo utasaidia madereva kupunguza makosa kwa kuhofia kutozwa faini kubwa.

Alisema wapo madereva wanaofanya makosa yale yale kila siku, jambo ambalo linatokana na kutambua kuwa hata wakitozwa faini watamudu kulipa.

“Tunataka kumaliza makosa ya barabarani. Tumelijadili jambo hili na tumeanza mchakato wa kuongeza faini,” alisema.

Alisema baadhi ya makosa hayo ni kuendesha gari huku dereva anazungumza na simu, sambamba na kiwango cha ulevi ambacho madereva hukutwa nacho, “tunataka kiwango kinachotambulika sasa, kuwa dereva akikutwa nacho ataonekana amelewa, kipungue zaidi.”

Wakati Mpinga akieleza hayo, mwaka jana kikosi hicho kilitoa jarida lililoainisha makosa 20 ya usalama barabarani na adhabu zake, huku faini ikiwa ni kati ya Sh 15,000 hadi Sh 50,000 na kifungo cha kati ya miezi sita hadi miaka miwili au vyote pamoja.

Desemba mwaka jana, Kamanda Mpinga aliliambia gazeti hili, kuwa adhabu za makosa hayo zinawachanganya wananchi, kutokana na tafsiri tofauti, kwamba wapo kwenye mchakato wa kutoa mchanganuo mwingine.

Lakini jana Mpinga alisisitiza: “Tumependekeza mchakato wa mabadiliko ya sheria yote ya usalama barabarani, tumeona tuzidishe faini. Kwa sasa faini yetu ni ile ile ya Sh 30,000 labda tukipeleka mahakamani inabadilika kutokana na uamuzi wa Mahakama.”

Kuhusu operesheni mbalimbali, Mpinga alisema ukaguzi na ukamataji bado vinaendelea ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kasi ya mabasi na magari inalingana na kasi iliyopangwa sehemu husika.

Akizungumzia kuongezwa adhabu za makosa barabarani,  Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Daladala (Darcoboa), Sabri Mabrouk alisema madereva ni lazima wafuate sheria bila shuruti.

"Naunga mkono huo mchakato wa kuongeza faini kwa madereva ambao wanakiuka sheria, kwani lazima dereva afuate sheria na taratibu za barabarani kutokana na ajali nyingi kutokea kwa uzembe wa madereva na watu wamekuwa wakishindwa kufuata sheria kwa kuzizoea," alisema.

Aliongeza kuwa sheria ikiwekwa mkazo, madereva wataepuka na kuenenda sawa na makosa mengi yataepukwa na barabarani kutakuwa hakuna shida yoyote.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo