Possi: Nitajiuzulu uwaziri


*Ni baada ya kuteliwa kuwa balozi
*Asisitiza hakuna Katiba kukiukwa

Salha Mohamed

Dk Abdallah Possi
NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wenye Ulemavu, Dk Abdallah Possi, amesema wakati wowote atakabidhi barua ya kujiuzulu ubunge kwa Spika Job Ndugai.

Hatua hiyo inakuja siku moja baada ya Rais John Magufuli kumteua kuwa balozi.

Dk Possi ambaye pia ni mwanasheria aliweka wazi jana kuwa hakuna sheria itakayovunjwa kutokana na uteuzi wake kuwa balozi na kuwatoa hofu Watanzania.

Kauli ya Dk Possi kuwa ataandika barua ya kujiuzulu ubunge imekuja wakati kuna mjadala mkubwa ukidai kuwa uteuzi wake umetokana na hoja za kisheria kwamba Katiba ilikiukwa baada ya Rais kuteua wabunge wawili; Abdallah Bulembo na Profesa Palamagamba Kabudi.

Baada ya uteuzi wa wabunge hao juzi, Mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu aliueleza umma kuwa watakwenda kupinga bungeni wateule hao, kwani kikatiba Rais kwenye nafasi zake 10 za uteuzi anatakiwa ateue wabunge wanawake angalau watano, lakini waliopo sasa ni wawili na kubaki na nafasi mbili tu.

Hata kama angejaza nafasi hizo kwa kuteuia wanawake bado asingefikisha idadi ambayo inatakiwa na Katiba kwani wangekuwa wanne.

Wakati mjadala huo ukiendelea, juzi usiku, taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari ilisema Rais alimteua Dk Possi kuwa balozi, hatua iliyoonekana ni ya kutaka kutengeneza nafasi tatu kwa ajili ya kukamilisha idadi hiyo ya wanawake iwapo italazimika.

Akizungumza jana baada ya kuteuliwa na Rais, Dk Possi alisema hatua iliyopo mbele yake ni kuandika barua ya kujiuzulu na si vinginevyo kwa kuwa anaheshimu imani ya Rais kwake.

 “Inawezekana kuandika barua ya kujiuzulu hakuna anayenikataza kufanya hivyo,” alisema baada ya mwandishi wa habari hii, kutaka kufahamu kama ameshaiandika na kuiwasilisha kwa Spika Ndugai.

“Bado… inaweza ikawa niiandike sasa hivi (jana), kubwa ni kwamba siwezi kuendelea kuwa mbunge, kwa hiyo naweza kuandika barua leo (jana), kesho(leo) au Jumatatu,” alisema.

Alisema kwa uteuzi huo hawezi kuendelea kutumikia nafasi mbili kwa wakati mmoja.

Possi alisema kama alivyoteuliwa kutumikia wananchi, atawakumbuka kwani amewatumikia kwa mwaka mmoja na kujifunza mengi.

“Unapokuwa kwenye jamii, unakutana na watu na unapoondoka utawakumbuka lakini mwisho wa siku nilikuwa mtumishi nahudumia Taifa, hivyo hii ni nafasi nyingine ya kuhudumia nchi,” alisema.

Alisema katika mwaka mmoja amejifunza vingi na mawaziri, wabunge hivyo ataendelea kutumia aliyojifunza.

Alisema katika nafasi aliyoteuliwa, hajui atakutana na changamoto zipi mpya kwani atakutana na watu wengi katika kujifunza.

“Tusubiri kila kitu kitakuja kwa wakati wake na hakuna sheria itakayovunjwa, we subiri katika hiki kitakachoendelea, lakini hakuna Katiba wala sheria itakayovunjwa,” alisema.

Alisema Watanzania wasubiri siku chache zijazo kila kitu kitakuwa sawa.

Spika Ndugai alipotafutwa kufahamu kama amepokea barua ya kujiuzulu kwa Dk Possi, alisema kwa sasa yuko jimboni na kama kuna barua ataikuta bungeni.

“Mimi hata bungeni sipo, niko jimboni, kama kuna barua nitaikuta huko huko nitakapokwenda bungeni Januari 31,” alisema.

Kuteuliwa kwa Profesa Kabudi na Bulembo, kuliamsha hisia kwa baadhi ya watu kwamba kwa vyovyote Rais atafanya mabadiliko kwenye Baraza lake la Mawaziri, hatua ambayo hivi sasa haiepukiki kwani nafasi ya Possi itatakiwa kujazwa.

Uteuzi wa wawili hao ulifanya sasa Rais abaki na nafasi mbili za uteuzi lakini kutokana na Possi kuteuliwa kuwa balozi, inaongezeka moja ambapo kwa vyovyote kikatiba zitatakiwa kujazwa na wanawake, ili kutimiza matakwa ya ‘angalau’ watano.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo