Maandamano yagubika kuapishwa kwa Trump


WASHINGTON, DC, Marekani

DONALD Trump ameapishwa kuwa Rais wa 45 wa Marekani, na kurudia ahadi yake ya kuifanya nchi yake kuwa taifa lenye nguvu zaidi kuliko ilivyokuwa awali.

Hata hivyo, Trump ameapishwa wakati ambao nchi hiyo imegawanyika, ambapo jana maelfu ya wananchi waliandamana kupinga kuapishwa kwake. Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni, ni asilimia 40 ya Wamarekani ndio wanamuunga mkono.

Trump aliapishwa huku idadi ya wageni walioalikwa kuhudhuria sherehe hizo ikiwa ni nusu ya wale waliohudhuria wakati Rais aliyemaliza muda wake jana, Barack Obama alipoapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 2009.

Takribani watu milioni 1.8 walihudhuria sherehe za kuapishwa kwa Obama wakiwamo watu maarufu na wanamuziki, lakini mambo yashindwa kwenda sawa kwa Trump kutokana na sherehe zake kuhudhuriwa na wageni takribani 800,000.

Jana Polisi walipambana na kundi kubwa la wananchi waliokuwa wakiandamana na kuziba mitaa na barabara za majimbo mbalimbali nchini humo wakipinga kuapishwa kwa Trump kuwa rais wa nchi hiyo.

Trump ambaye alimshinda mpinzani wake wa Chama cha Democratic, Hillary Clinton katika uchaguzi mkuu uliofanyika Novemba 8 mwaka jana, amekuwa akipingwa na kundi kubwa la raia wa nchi hiyo ambao wanasema hakuwa chaguo lao bali alishinda kutokana na mfumo mbovu wa upigaji kura unaotumiwa na Taifa hilo.

“Tutaandamana tu wala hatutaogopa kama Polisi watatupiga au kutukamata, lengo ni kumwonesha Trump kwamba hakubaliki miongoni mwa raia wengi wa Marekani, haijalishi ameshinda na anaapishwa, katu hatopata nafasi nyoyoni mwetu.

“Hajawahi kuwa na sera zinazoonesha kama ni kiongozi wa kutazamwa, kauli zake za kibaguzi kuanzia rangi na wanawake vinamfanya kuwa Rais wa ajabu kuwahi kutokea Marekani,” alisema mmoja wa waandamanaji katika eneo la San Diego, California.

Democrats

Sherehe hiyo iligubikwa na mabadiliko mengi mahsusi tofauti na ilivyozoeleka kwa watangulizi wake.

Jambo kubwa mbali na maandamano hayo yaliyoendeshwa na wafuasi wa chama cha Democrats, ni uchaguzi wa Trump wa Biblia ambayo alitumia kuapia, kwani alichagua aliyotumia utotoni, lakini pia kiutaratibu alitumia Biblia ya Lincoln ambayo ilitumiwa katika viapo vitatu vilivyotangulia.

Biblia hiyo ilitumiwa na Abraham Lincoln mwaka 1861 na Barack Obama mwaka 2009 na mwaka 2013.

Tofauti na viapo vya nyuma, idadi ya waburudishaji haikuwekwa wazi kutokana na wengi waliokuwa wamejulishwa kushiriki walijijitoa kutokana na upinzani wa kisiasa uliogubika sherehe hizo.

Mmoja wa waburudishaji waliothibitishwa tangu awali ni Jackie Evanco (16) ambaye ni maarufu kwa albamu yake ya ‘America’s Got Talent’ na ndiye aliyeimba Wimbo wa Taifa.

Jambo lingine lisilo la kawaida ni idadi kubwa ya wajumbe wa Baraza la Congress wa Democrats ambao walitangaza kususa hafla hiyo, huku idadi ikionesha kuwa theluthi tatu ya wajumbe wote wa Baraza hilo kutoka Democrats hawakushiriki.

Hata hivyo ratiba ya matukio ya jana haikutofautiana sana na ilivyozoeleka katika viapo vilivyotangulia vya marais, hata hivyo, Trump ambaye alilala na familia yake kwenye jengo la Blair House mkabala na Ikulu ya White House, alianzia kanisani asubuhi.

Baadaye akifuatana na mkewe, Melania, walikwenda White House kufungua kinywa pamoja na familia ya Rais Barack Obama kabla ya kwenda Capitol.

Baada ya kiapo, Obama aliondoka na kumwacha Trump akipata chakula cha mchana kabla ya matukio mengine kama vile gwaride na shamrashamra zingine ili kuhitimisha siku hiyo.

Wapinzani

Wapinzani wa Trump usiku wa kuamkia jana walipambana na polisi na kunyunyiziwa pilipili jijini hapa.

Kundi kubwa la waandamanaji wanaompinga Rais Trump lilikusanyika mapema nje ya Klabu ya Taifa ya Waandishi wa Habari, ambako kulikuwa na sherehe zijulikanazo kama ‘DeploraBall’ – tukio ambalo liliandaliwa na wafuasi wa Trump juzi usiku.

Mamia ya waandamanaji hao waliingia mitaani nje ya klabu hiyo, wengi wakiimba huku wakibeba mabango ya kumkataa Trump.

Mmoja wa wafuasi wa Trump ambaye alikuwa eneo hilo lakini hakuhudhuria hafla hiyo, alidai kuwa waandamanaji hao walifanya vurugu – wakimshutumu mmoja wao kwa kumshambulia kwa mlingoti wa bendera.

“Nilikuwa nimevalia kofia yangu yenye maandishi ya ‘Ifanye Marekani Taifa Kubwa tena’, na mwanamume mweupe akanifuata kwa nyuma na kunisukasuka kwa mlingoti wa bendera – nikapoteza fahamu kama dakika moja hivi,” Jones Allsup (21) aliiambia Fox News.

Wafuasi

Kambi ya Trump kwenye ghasia hizo nayo iliwakilishwa na waendesha mapikipiki waliotoka sehemu mbalimbali za nchi kuja hapa siku kadhaa kabla ya jana ambao walijiandaa kukabiliana na waandamanaji hao.

Kundi hilo linalojiita Bikers For Trump liliomba kibali cha watu 5,000 kukaa kwenye bustani ya John Marshall, huku wakipanga kufanya mkutano usio rasmi kati ya tukio la kula kiapo na kuanza kwa gwaride.

Muasisi wa kundi hilo, Chris Cox (48), aliiambia Fox & Friends: “Kwenye tukio hili ambalo tunahitajika, tutajenga ukuta wa nyama. Tutakuwa bega kwa bega na ndugu zetu na tutakuwa kidole kwa kidole na yeyote atakayethubutu kuvuka vizuizi vya Polisi,” alionya Cox.

Kabla ya kuapishwa Trump na Makamu wake, Mike Pence na familia zao walihudhuria ibada kwenye Kanisa la Mt John baadaye wakaenda Ikulu ya White House kufungua kinywa na familia ya Rais Barack Obama kabla ya kuelekea jengo la Capitol, kuapishwa na Jaji Mkuu, John Roberts Jr na kuhudhuriwa na wabunge wa Baraza la Congress.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo