Jecha avunja ukimya


Suleiman Msuya

Jecha Salim Jecha
BAADA ya kimya cha muda mrefu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, amevunja ukimya akieleza kuwa tangu Mapinduzi ya Zanzibar, nchi hiyo haijawahi kufanya uchaguzi usio na misuguano.

Aidha, amesema asingetaka kuzungumzia uamuzi wa ZEC kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka juzi kwa kuwa hilo lina historia ndefu na angependa kwanza ikamilike ripoti ya mchakato wa uchaguzi huo.

Jecha alisema hayo alipokuwa akizungumza kupitia Kipindi cha Funguka kilichorushwa na Kituo cha Azam kikiongozwa na mwandishi mkongwe nchini, Tido Mhando.

“Historia inaonesha kuwa Zanzibar tangu Mapinduzi hatujawahi kufanya uchaguzi ukaisha kwa amani, hivyo ni jambo ambalo linapaswa kufanyiwa kazi ili kuhakikisha kuwa dhana hiyo inaondoka,” alisema.

Alisema katika uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka 2015 mchakato wa kupiga kura ulienda vizuri, ila tatizo lilikuja wakati wa majumisho.

“Kusema kweli uchaguzi ulifanyika vizuri ila kulikuwa na dosari mbalimbali ambazo zililalamikiwa na baadhi ya vyama vya siasa, hivyo nililazimika kufanya nililichokifanya pamoja na kuonekana peke yangu ila ni maamuzi ya ZEC,” alisema.

Alisema kwenye Tume mgawanyiko unaweza kutokea hasa ukizingatia mfumo wa Tume ya Zanzibar ambayo inashirikisha vyama.

Mwenyekiti huyo alisema changamoto kubwa katika uchaguzi wa mwaka 2015 zilionekana katika upande wa Pemba ambako watendaji walionekana kukiuka baadhi ya taratibu.

“Wakati matokeo ya Unguja yanaingia hakukuwa na matatizo, ila yalipoanza kuingia matokeo ya Pemba tulianza kuona ukiukwaji wa taratibu hasa katika masuala ya kiufundi, hakukutokea vurugu, lakini kulitokea mapungufu yaliyonisukuma kufanya nilichofanya,” alisema.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa kasoro hizo za matokeo ya uchaguzi Zanzibar, hazijaonekana kwa upande wa wagombea wa Muungano kwa sababu hisia za uchaguzi zipo upande wa Zanzibar.

Alisema viongozi wa kisiasa na wananchi katika kisiwa hicho wamejawa na jazba za kisiasa hali ambayo inachangia kuwepo kwa mtafaruku.

Kwa nini alifuta matokeo?

Kuhusu sababu za kufuta matokeo, alisema ataziainisha katika ripoti hiyo, ambayo imebainisha kila kitu huku akisisitiza kuwa utaratibu ulifuatwa katika uamuzi huo.

Jecha alikanusha taarifa kuwa uamuzi huo wa kufuta matokeo ulitokana na maagizo ya Rais Dk. Ali Mohamed Shein, huku akisisitiza kuwa hata namba yake ya simu hana.

Alisema historia inaonesha kuwa uchaguzi Zanzibar umeshafutwa, hivyo isionekane jambo jipya na kubainisha kuwa iwapo kutakuwepo na mfumo bora zaidi yeye yupo tayari kufanya nao kazi kwa maslahi ya Zanzibar na Wazanzibari.

Mwenyekiti huyo alisema katika uamuzi wake hakupendelea chama chochote, ila alifuata taratibu na kama angependelea angeweza kutangaza ushindi na si kurudiwa kwa uchaguzi.

“Ukiwa kiongozi kuna wakati unalazimika kuchukua maamuzi mazito, kwani huwezi kuona jahazi inazama unaacha kuchukua maamuzi kisa kusubiri watu wafanye uamuzi huku wengine wakifa,” alisema.

“Narudia kama kiongozi ukikabidhiwa jambo lolote si lazima usubiri maamuzi ya vikao unatakiwa kuchukua hatua na ndivyo nilivyofanya,” alisema.

Amzungumzia Maalim Seif

Jecha pia alisema kitendo cha aliyekuwa mgombea wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kutangaza matokeo hayo kilikuwa kinyume na sheria na taratibu.

Alisema matokeo ambayo Hamad alitangaza yalikuwa batili, hayakuwa sahihi yalikuwa yamepikwa na yalikiuka taratibu hivyo kuvitaka vyombo husika kufanyia kazi na si tume.

“ZEC haikumuonea Seif ila mambo ambayo yalifanyika hayakuwa sahihi ni ngumu kuvumilika,” alisema

Ilivyokuwa Oktoba 28, 2015

Jecha alisema kuwa uchaguzi huo haukuwa wa haki na kwamba kulikuwa na ukiukaji mkubwa wa sheria za uchaguzi.

Alisema baadhi ya makamishna wa tume hiyo, badala ya kutekeleza majukumu yao inavyotakiwa kikatiba "wamekuwa ni wawakilishi wa vyama vyao".

"Kumegundulika kasoro nyingi katika uchaguzi huu miongoni mwa hizo ni kubainika kwa baadhi ya vituo hasa Pemba vimekuwa na kura nyingi kuliko daftari la wapiga kura wa kituo husika."

Alisema hilo ni jambo la kushangaza ikizingatiwa kwamba "baadhi ya wapigakura hawakwenda kuchukua vitambulisho vyao vya kupigia kura".

Kadhalika, alisema kura hazikupata ulinzi mzuri hususan kisiwani Pemba ambako alisema kuwa baadhi ya mawakala wa baadhi ya vya vyama vya siasa katika kisiwa hicho walifukuzwa.

Aliongezea kuwa vijana katika eneo hilo walivamia vituo vya kupigia kura kwa lengo la kutaka kuzua ghasia, na pia vyama vya siasa vilionekana "kuingilia majukumu ya tume ikiwemo kujitangazia ushindi na kupelekea mashindikizo kwa tume."

"Nimeridhika kwamba uchaguzi huu haukiwa wa haki na kuna ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu za uchaguzi," alisema.

"Hivyo, kwa uwezo nilionao natangaza rasmi kwamba uchaguzi huu na matokeo yake yote yamefutwa na kwamba kuna haja ya kurudia uchaguzi huu."
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo