Mvua yaua mmoja, yaezua nyumba 49


Salum Maige, Geita

NYUMBA 49 zimeezuliwa na kubomolewa huku Neema Masunga (27) akipoteza maisha kwa kupigwa na radi kutokana na mvua iliyoambatana na upepo na radi kunyesha kwenye machimbo ya Matabe kijijini Bwanga wilayani Chato mkoani hapa.

Katika tukio hilo, la juzi nyumba 11 zilibomolewa na 38 kuezuliwa mapaa na kusababisha familia kukosa mahali pa kuishi na wengine kulazimika kujihifadhi kwa majirani.

Tukio hilo lilitokea saa mbili usiku baada ya mvua iliyoambatana na upepo mkali na ngurumo za radi kunyesha kwa nusu saa.

Mwenyekiti wa eneo hilo, Jackson Kusekwa alisema marehemu Neema ameacha watoto watano, mmoja akiwa wa wiki mbili.

Alisikitishwa na tukio hilo lililotokea kwenye kipindi kigumu cha njaa kwa waakzi wa Matabe baada ya mazao waliyolima yakiwamo mahindi kukauka kwa jua.

Alisema Neema alipoteza maisha baada ya kupigwa na radi akiwa chumbani akimnyonyesha mwanawe huyo ambapo radi ilimrusha hadi sebuleni na kufariki dunia.

“Radi ilimrusha hadi sebuleni na mtoto akabaki chumbani…imeharibu sana nyumba kwani imepasuka, kwa ujumla tuna hali mbaya sana, wananchi kwa sasa wanaishi kwa shida wengine wamehamia kwa majirani ili kujihifadhi baada ya nyumba zao kubomolewa,” alisema Kusekwa.

Mmoja wa wanakijiji, Abel Charles alisema baada ya hali hiyo wananchi walikusanya mabati yaliyoezuliwa na katika harakati hizo walipata taarifa za mtu kufariki dunia na ndipo wananchi walijikusanya na kwenda eneo la tukio na kushuhudia mwanamke huyo akiwa amepoteza maisha.

Mama mzazi wa marehemu, Mariam Masunga (78) alisema, binti yake amemwachia watoto hao na mdogo kabisa anayehitaji msaada kwani hata yeye kwa umri wake alikuwa akimtegemea mwanawe huyo.

“Naomba msaada wa kulea watoto hawa...mimi sina uwezo, kwani nimezeeka katika maisha yangu nilikuwa namtegemea mwanangu ambaye sasa amefariki dunia, naiomba Serikali inisaidie,” alisema Mariam huku akiangua kilio.

Aidha, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Chato ambaye ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Shabaan Ntarambe alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai kuwa alituma wajumbe wa kamati yake kufuatilia kabla ya kutoa taarifa hizo.

“Nimemtuma OCD (Mkuu wa Polisi Wilaya) kufuatilia hilo tukio; ni kweli limetokea akishatoka huko nitatoa taarifa baadaye,” alisema Mkuu wa Wilaya.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo