Walimu wakuu 63 washushwa vyeo Mtwara


Suleiman Msuya

Halima Dendegu
SIKU mbili baada ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), kutangaza matokeo ya kidato cha pili na shule tisa za mkoa wa Mtwara kushika mkia, Mkuu wa Mkoa huo, Halima Dendegu ameagiza mamlaka husika kuwavua vyeo walimu wakuu wa shule za msingi 63 kutokana na matokeo hayo.

Akizungumza na JAMBOLEO juzi Dendegu alisema alichukua aumuzi huo baada ya kujiridhisha kutokana na utafiti ambao waliufanya baada ya matokeo ya darasa la saba yaliyotoka mwaka jana.

Alisema taarifa zilizopo zinaonesha wanafunzi hao wa kidato cha pili waliofeli walifanya vizuri kwenye matokeo ya darasa la saba hali ambayo inaibua maswali mengi katika kufeli huko.

Mkuu huyo alisema zipo changamoto mbalimbali ambazo zipo pia katika mikoa mingine ila Mtwara zimekuwa zikitumiwa kama sababu za changamoto za mitihani.

“Hawa wanafunzi walifaulu mtihani wa darasa la saba mwaka 2014/15 hivyo ni jambo la kushangaza kuona leo wanafeli, lazima kuna uzembe kwa wasimamizi wa watoto hao katika ngazi ya msingi,” alisema.

Alisema baada ya kuhoji baadhi ya walimu, walidiriki kusema kuwa walitoa majibu kwa wanafunzi hao hali ambayo ilichangia ufaulu, hivyo kusababisha kilichotokea.

Mkuu wa Mkoa alisema pamoja na walimu wakuu hao kushushwa vyeo, bado wanaendelea na mkakati wa kubaini udhaifu wa walimu wa sekondari na pia maofisa elimu ili wajiandae kuwajibika.

Dendegu alisema zipo changamoto kama ufundishaji wa mazoea, kufanya mambo kwa kufupisha, utoro kwa wanafunzi, wazazi kukosa mwamko na zingine nyingi.

Alisema pamoja na changamoto hizo, wana mikakati ya kutoa chakula na kutaka maofisa elimu kufuatilia shule mbalimbali lakini bado uzembe upo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo