Walia Bodi ya Mikopo kuwakata 15%


Hussein Ndubikile

WANUFAIKA wa mikopo ya elimu ya juu wameiomba Serikali kuangalia upya sheria  ya makato ya asilimia 15 ya mshahara wanayokatwa na waajiri ili kubaki na kipato cha kutosha kujikimu kimaisha.

Awali Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini (HESLB) ilikuwa ikiwakata asilimia 8 wanufaika walioajiriwa lakini mwaka jana Bunge lilipitisha sheria mpya inayomtaka mwajiri amkate mwajiriwa asilimia hiyo na wanufaika wasio kwenye ajira rasmi kutakiwa kulipa asilimia 10 ya kipato chao.

Kauli hiyo ilitolewa juzi Dar es Salaam kwenye msako wa ofisi kwa ofisi unaoendeshwa na Bodi hiyo na mnufaika ambaye pia ni Ofisa Mkuu wa Ubora wa Bidhaa zinazozalishwa wa kampuni ya Tanzania Leather Limited.

Alisema kiasi cha makato hayo kilichoanza kutekelezwa Novemba mwaka jana hakijaangalia hali halisi ya mishahara wanayolipwa wanufaika wenye kiwango cha Astashahada na Shahada kwenye kampuni binafsi na mwajiriwa akikatwa na kujumlisha makato mengine, hubaki na kiasi kidogo cha fedha kisichokidhi mahitaji muhimu.

“Hebu angalia mtu labda anapata mshahara wa Sh 400,000 anakatwa kodi, NSSF, bima na hiyo asilimia 15 unabaki na fedha ndogo ambazo ni vigumu kumudu gharama za maisha,” alisema.

Alisema hakatai mtu anapochukua mkopo anakuwa na jukumu la kurejesha ila analalamikia kiwango kikubwa kilichopitishwa na wabunge bila kuangalia hali ya maisha ya sasa ilivyo.

Meneja Urejeshaji Mikopo wa Bodi hiyo, Deodatus Mwiliko alisema walilazimika kupendekeza kiwango hicho kutokana na baadhi ya wanufaika kudaiwa fedha nyingi hivyo asilimia 8 isingewasaidia kurejesha kwa haraka.

“Kuna wanufaika wanadaiwa hadi Sh milioni 60 ukisema uwakate kwa kutumia asilimia 8 huwezi kumaliza deni inaweza ikatokea mtu anastaafu bila kumaliza deni ilikuwa akatwe kwenye NSSF,” alisema.

Alisisitiza kuwa uamuzi huo umefanyika kuwarahisishia wanufaika kulipa madeni yao kwa wakati.

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Urejeshaji Mikopo wa HESLB, Phidelis Joseph alisema waajiri watakaobainika kutowasilisha majina ya wanufaika kwa wakati watatozwa faini na kuhukumiwa kifungo cha miezi 36 jela.

Meneja Rasilimali Watu wa Kampuni ya Kamal Steels Ltd, Joseph Bryceson aliwaomba waajiri kuwasilisha taarifa ya majina ya wanufaika kwa wakati kwa ajili ya kusaidia urejeshaji mikopo ili wengine wenye uhitaji wanufaike.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo