JPM aombwa ajira ya wahadhiri wenye PhD


Edith Msuya
MTAALAMU wa elimu na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Kitila Mkumbo, amemwomba Rais John Magufuli aruhusu ajira za walimu wa vyuo vikuu nchini na hasa wenye kiwango cha Shahada ya Uzamivu (PhD) ili kunusuru elimu ya vyuo vikuu.
Profesa Kitila Mkumbo

Amesema hali iliyopo sasa ni changamoto kubwa ya uhaba wa walimu hao kwenye vyuo vikuu nchini ikiwamo UDSM na kwa hali hiyo wanafunzi wa vyuo vikuu wengi wao wanafundishwa na walimu wasiokuwa na PhD.

Profesa Mkumbo alitoa kauli hiyo Dar es Salaam jana wakati wa uzinduzi wa Mpango Mkakati wa HakiElimu wa mwaka 2017 hadi 2021 ambapo wadau wa elimu walipata fursa kujadili mafanikio na changamoto ambazo zinakwamisha ukuaji elimu nchini.

Akiwasilisha mada, Profesa Mkumbo alisema zipo changamoto nyingi na kwenye elimu ya juu, kuna uhaba mkubwa wa walimu wenye PhD ambao ndio walipaswa kuwapo kufundisha wanafunzi hivyo kukosekana wa kutosha kumesababisha walimu kuwa na wahadhiri wasaidizi wengi.

Alisema kwa mazingira hayo wahadhiri waandamizi ni wachache na matokeo yake wasaidizi inabidi wawe wanaendelezwa kitaaluma hadi kufikia sifa ya PhD na hicho ndicho kinafanyika sasa.

Alitolea mfano kuwa hata UDSM wahadhari waandamizi wenye PhD ni wachache huku akieleza kuwa pamoja na uchache huo, Rais Magufuli amekuwa akiteua wasomi hao serikalini na hivyo kuongeza uhaba wa walimu wenye sifa kwenye chuo hicho.

Alisema ili kukabiliana na uhaba wa wahadhiri wenye PhD UDSM ni vema Rais akaruhusu ajira za walimu wenye kiwango hicho ili kuendelea kuzalisha na kupima wasomi ambao watakuwa msaada kwa Taifa.

Alifafanua kuwa UDSM kuna asilimia 41 ya wahadhiri wenye PhD huku vyuo vingine hali ikiwa ni mbaya.  

Alisema mbali ya uhaba huo kwenye vyuo vikuu, pia kuna changamoto ya mfumo mzima wa elimu nchini kuanzia msingi, sekondari hadi elimu ya juu.

Profesa Mkumbo alisema elimu ya msingi haandai mwanafunzi kuwa na maarifa na kibaya zaidi hata wanaotoa elimu hiyo wengi wao wamejikita kuangalia mwanafunzi anafaulu kwa alama gani, badala ya mwanafunzi kupata maarifa ya aina gani ya kumsaidia kwenye maisha yake na Taifa kwa jumla.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo