Wabunge wajipanga kuibana Serikali



Mwandishi Wetu

SIKU 10 kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Sita wa Bunge, wabunge kutoka mkoa wa Pwani, Lindi na Mtwara wameunda umoja wa kuibana Serikali bungeni wakitaka kupewa majibu ya kueleweka kuhusu suluhisho la migogoro kati ya wakulima na wafugaji nchini.

Taarifa zilizolifikia gazeti hili kutoka kwa watu wa karibu wa wabunge hao, huku baadhi yao wakithibitisha na kutotaka majina yao kuandikwa gazetini, zinaeleza kuwa uamuzi huo unatokana na migogoro ya makundi hayo kutopatiwa ufumbulizi, licha ya kuwepo muda mrefu na kusababisha wananchi kupoteza maisha.

“Sisi wabunge lazima tusimame katika nafasi yetu ya kutetea wananchi bila kujali itikadi za vyama vyetu,” alisema mbunge mmoja kutoka mkoa wa Pwani.

Habari hizo zinaeleza kuwa wazo hilo lililowaunganisha wabunge wa CCM, Chadema na CUF liliibuliwa na wabunge wa mkoa wa Pwani  na kuungwa mkono na wenzao wa mikoa ya Mtwara na Lindi.

Februari mwaka jana katika mkutano wa Bunge mjini Dodoma, wabunge wanaotoka kwenye mikoa ambayo Reli ya Kati inapita, waliunda umoja kama huo, lakini wao walikuwa wakishinikiza ujenzi wa reli hiyo, wakisema bila Serikali kusikiliza kilio chao, watahamasisha wenzao waisusie bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/17.

Kufuatia sakata hilo, Serikali ilitoa majibu kuhusu ujenzi huo ikiwa ni pamoja na kutaja kiasi cha Sh trilioni 1 kilichotengwa kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge).

“Ushawishi umekuwa mkubwa na tumeungwa mkono na wabunge wengine wa mkoa wa Morogoro. Bado tunaendelea kushawishi wengine ili wawe pamoja na sisi. Migogoro hii inawaumiza wananchi, lakini Serikali imekaa kimya bila kuja na mkakati wa kueleweka,” alisema mmoja wa wabunge kutoka mkoa wa Mtwara.

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba alipoulizwa kuhusu mkakati wa wabunge hao alisema, “Kwa sasa Serikali ipo kazini jambo hili la migogoro ya wakulima na wafugaji linafanyiwa kazi. Kuhusu mkakati wa wabunge hao siujui kwa kweli ila nitakutana nao bungeni na tutakuwa na majibu ya kutosha kuwaridhisha.”

Mmoja wa wabunge hao kutoka Chadema alisema Serikali haina dira wala mwelekeo kwa maelezo kuwa wakulima na wafugaji wamekuwa wakiuana lakini hakuna waziri anayesema lolote na kusisitiza, “watatueleza ndani ya bunge kazi yao ni nini.”

Katika mapendekezo hayo, wabunge hao ambao wamekuwa wakijadili jambo hilo mara kwa mara sambamba na kupanga mikakati, wameshauriana kuishauri Serikali kuipeleka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi chini ya Ofisi ya Rais kwa usimamizi zaidi.

“Tatizo la wakulima na wafugaji halina mwenyewe. Leo linaweza kutokea jimbo hili na kesho likatokea jimbo jingine. Si suala la huyo wa Chadema au huyu wa CCM. Lazima tuungane kuhakikisha suluhisho linapatikana,” alisema mbunge wa CCM mkoa wa Lindi.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo