Sekta binafsi hatarini kuuawa kiuchumi


Charles James
David Kafulila

WAKATI Mbunge wa zamani wa Kigoma Kusini, David Kafulila, akiiponda ripoti ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), kuhusu hali ya uchumi nchini, wachumi wamejitokeza kuichambua huku wakisema Serikali iko hatarini kuua sekta binafsi.

Ripoti hiyo ya IMF ilitolewa Jumanne ikiipongeza Serikali kwa kuimarisha uchumi, kudhibiti mfumuko wa bei, kupunguza pengo linalotokana na ununuzi wa nje ya nchi huku ikitoa hadhari kuwa Taifa linakabiliwa na hatari itakayozuia kuendelea kukua kwa uchumi wa sekta binafsi.

Akitolea ufafanuzi ripoti hiyo juzi, Kafulila alisema ripoti imeendelea kusisitiza eneo la ukuaji uchumi kwa kasi nzuri ya asilimia saba, jambo ambalo alisisitiza kuwa ukuaji huo upo tangu mwaka 2005/06 ambapo uchumi ulirekodiwa kukua kwa asilimia 6.9 kwa mujibu wa hotuba ya Bajeti ya mwisho ya utawala wa Rais Benjamin Mkapa, hivyo si jambo jipya.

Alisema pia ilisisitiza kuhusu mafanikio kwenye ukusanyaji kodi kwamba wastani wa makusanyo umeongezeka kutoka Sh bilioni 800 kwa mwezi hadi Sh trilioni 1.1 kwa mwezi, huku mapambano dhidi ya ufisadi  yakionekana ingawa bado kuna changamoto ya kujenga mfumo wenye nguvu ili vita iyo iwe endelevu.

Alisema ripoti hiyo ilionesha kwamba nakisi kwenye akaunti ya biashara kimataifa imeshuka jambo ambalo ni jema na la afya kiuchumi, lakini ripoti hiyo inakwenda mbali zaidi kuonesha kwamba nakisi hiyo imeshuka kutokana na kupungua kwa uagizaji wa malighafi za viwanda.

“Ingekuwa nakisi imeshuka kwa kupunguza uagizaji wa bidhaa zisizo za uzalishaji ingekuwa afya, lakini kushuka kwa nakisi hiyo kunakotokana na kushuka kwa uagizaji wa bidhaa muhimu kwa uzalishaji viwandani ni kasoro hasa katika mazingira ambamo Serikali inatengeneza uchumi wa viwanda,” alisema Kafulila.

Akizungumzia ukata, alisema ripoti ilisisitiza kuwa uchumi unakabiliwa na ukata, na kwamba kutatua hilo, Serikali inapaswa kuhakikisha sekta binafsi inapata mikopo ili kuchangamsha biashara, jambo ambalo ni changamoto kubwa hasa kutokana na uamuzi   wa kukopa benki za ndani kiasi cha Sh bilioni 1,200 ili kugharimia bajeti.

Profesa Tolly Mbwete wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema ripoti hiyo haiendani na namna ambavyo wananchi wamekuwa wakilalamika kuhusu ugumu wa maisha uliopo sasa, jambo ambalo lilitokana na Serikali kuminya mianya ya upatikanaji fedha.

Alisema sera ya Serikali kubana matumizi ni wazi inaweza kuchangia kushuhudia kundi kubwa la wawekezaji wakifunga ofisi zao, kwani zimekuwa zikikosa wateja, “mathalan hoteli binafsi nyingi hivi sasa tunaona zikifungwa kwa kukosa wateja na hiyo ni kwa sababu Serikali imeagiza watendaji wake kutumia za Serikali.

“Na ndiyo maana IMF imesema kuna hatari kwenye sekta binafsi na utaona ni kiasi gani hali si nzuri huko, kampuni nyingi zinafungwa, hoteli zingine zinageuzwa hosteli, matokeo yake tunapokea kundi kubwa la watu wasio na ajira uraiani, jambo ambalo linaweza kuongeza wezi mitaani,” alisema Profesa Mbwete.

Mhadhiri wa Uchumi wa UDSM, Haji Semboja alisema ripoti hiyo haisemi ukweli uchumi gani umekua, kwani huu inaosemea ni wa kawaida na umedumu kwa miaka 15 bila kubadilika kutokana na nchi yetu kutokumbwa na ukame maeneo mengi.

“Kuna kitu kwenye uchumi kinaitwa ‘micro’ ambayo ni namna hali ya wananchi ilivyo na IMF imekuwa ikitoa ripoti hizi katika nchi masikini na ndiyo maana inasema bei isipande kutokana na asilimia 70 ya wananchi kuishi vijijini na ni wakulima,” alisema.

Semboja alisema ripoti ya IMF inaonesha kuwa Serikali hailengi kunufaisha watu binafsi na ndiyo maana ikarudisha wamachinga barabarani, jambo linaloua wenye maduka ambao wanalipa kodi, kwa sababu wateja wengi wanadakwa na wamachinga nje ya maduka na kuwauzia bidhaa kwa bei rahisi huku wakiwa hawana risiti hivyo kukwepa kodi.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo