Hatima ya mjane wa bilionea Msuya Januari 23


Grace Gurisha

Mariam Mrita
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam Januari 23 inatarajia kutoa uamuzi wa kumwacha au kutomwacha huru mjane wa bilionea Erasto Msuya, Mariam Mrita (41) na mwenzake.

Hiyo inatyokana na upande wa Jamhuri kushindwa kurekebisha hati ya mashitaka dhidi yake.

Uamuzi huo utatolewa na Hakimu Mkazi Godfrey Mwambapa baada ya Wakili wa Serikali, Mutalemwa Kishenyi na wakili wa utetezi, John Malya kutoa hoja za kisheria kutokana na kwamba kila mmoja anavutia kwake.

Kishenyi alidai kuwa walishindwa kufanya marekebisho kama Mahakama ilivyoamuru, kwa sababu muda wa siku mbili waliokuwa wamepewa ulikuwa mfupi, kwa hiyo akaomba kupewa muda Zaidi, ili kurekebisha kwa kuwa suala la hati linahitaji umakini.

Hata hivyo, Malya alidai kuwa amri iliyotolewa mahakamani hapo ni ya kisheria, hivyo  upande wa Jamhuri ulitakiwa kutekeleza ama kukata rufaa, lakini ulishindwa kufanya hivyo.

Kutokana na upande wa Jamhuri kushindwa kutekeleza amri hiyo, aliiomba Mahakama iwaache huru washitakiwa kwa sababu hakuna hati sahihi ya mashitaka inayowafanya waendelee kushitakiwa.

Akijibu hoja hiyo, Mutalemwa alidai kuwa hawajashindwa kuleta hati hiyo, lakini kama alivyosema awali kuwa anaomba muda zaidi na kutokana na hilo, wataieleza Mahakama kama watakata rufaa au la.

Januari 9 Mahakama hiyo iliamuru upande wa Serikali ubadilishe hati ya mashitaka ndani ya siku mbili ambapo  alisema uamuzi huo ulitokana na kupitia hoja za pande zote mbili na kubaini kuwa hati ya mashitaka ina upungufu sehemu mbili ukiwamo wa kutoonesha kama kuna mtu aliyesababisha kifo cha mtu mwingine.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, Miriam na Revocatus Muyela wanadaiwa kumuua kwa makusudi dada wa bilionea, Msuya, Aneth Msuya kwa kumchinja nyumbani kwake eneo la Kibada Kigamboni, Dar es Salaam Mei 25 mwaka jana.

Miriam ambaye ni mshitakiwa wa kwanza wa kesi hiyo ni mjane wa bilionea Msuya ambaye aliuawa kwa risasi Agosti mwaka juzi Mijohoroni kando ya barabara ya Arusha – Moshi wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo