Mtatiro, Kambaya waanika ufujaji wa mamilioni ya CUF


Celina Mathew

Julius Mtatiro
MGOGORO wa CUF umechukua sura mpya, baada ya kila upande kuanza kutoa siri za ndani za matumizi mabaya ya mamilioni ya rukuzu za chama hicho.

Aliyeanza kuweka wazi siri hizo hadharani ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi CUF, Julius Mtatiro, anayeunga mkono upande Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye alieleza namna ruzuku ya Sh milioni 369, ilivyochukuliwa kinyume na taratibu.

Juzi Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma CUF, Abdul Kambaya, anayeunga mkono upande wa Mwenyekiti, Profesa Ibrahim Lipumba, aliamua kuweka hadharani uchotaji mwingine wa mamilioni ya chama hicho unaodaiwa kufanywa na Mtatiro na kujibiwa.

‘Uchotaji’ wa Mtatiro

Kambaya katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, alidai kuwa Mtatiro alipokuwa Naibu Katibu Mkuu Bara, aliwahi kuingizia zaidi ya Sh milioni 108 za chama hicho kwenye akaunti yake iliyopo NMB, yenye namna 5091603335.

Kwa mujibu wa madai ya Kambaya, Septemba 5 mwaka 2011 Mtatiro alianza kutoa fedha hizo kidogokidogo, kwa kuhamisha Sh milioni 34.09; Septemba 13, 2011 alihamisha Sh 270,000 na Septemba 19, 2011 alihamisha Sh. milioni 24.87.

Kambaya aliendelea kudai kuwa Septemba 27, 2011 Mtatiro, alihamisha Sh milioni 30.87 na Septemba 30, 2011 kiongozi huyo alihamishsa Sh milioni 10,85 huku Oktoba 3 akihamisha Sh. milioni nane na kumaliza kuhamisha Sh 108,959,500.

"Huyu ndie Julius Mtatiro ambae anataka kujifanya mtakatifu kumbe ndie mtakatishaji namba moja wa fedha za CUF. Je wakati Julius anahamisha fedha hizi kutoka akaunti ya CUF na kuingiza kwenye akaunti yake binafsi, alikua hujui kwamba fedha za taasisi haziruhusiwi kuhamishiwa kwenye akaunti binafsi? Alihoji.

Akitoa ufafanuzi kuhusu akaunti namba 414016000207 ya Mhina Omary Masoud iliyopo NMB, Kambaya alidai mwaka 2012 Mtatiro alipokuwa Naibu Katibu Mkuu Bara, alimwingizia mtu huyo huyo Sh milioni 47.

Kambaya alisema uwekaji wa fedha za ruzuku za CUF katika akaunti ya Mhina Omary Masoud, haukuwa jambo geni kiasi cha kumfanya Mtatiro ashangae na kujifanya hamjui mwenye akaunti hiyo.

Kiongozi huyo anayeunga mkono ypande wa Lipumba, alidai kuwa Mtatiro anajua kuwa akaunti hiyo pia ili wahi kupatiwa fedha chini ya uongozi wake lakini hukuwahi kuitisha mkutano wa vyombo vya habari na kuelezea umma juu ya ukiukwaji huo wa taratibu za fedha za taasisi.

Alidai katika taarifa yao kwa vyombo vya habari kuhusu kadhia hiyo, walisisitiza kuwa Mtatiro si kiongozi wa CUF, hivyo si sahihi yeye kutoa taarifa kuwa CUF imeibiwa mamilioni na pia haikua sahihi kusema fedha hizo zimeibwa kutoka Hazina.

"Julius Mtatiro na genge lake ni wapiga dili waliokosa nafasi ya kutimiza matakwa yao ndani ya CUF na si miongoni mwa viongozi wanao weza kuwa waadilifu,"aliongeza Kambaya.

‘Uchotaji’ wa Kambaya

Akijibu tuhuma dhidi yake zilizotolewa na Kambaya, Mtatiro naye aliamua kuanika namna Naibu Mkurugenzi huyo wa Habari, vyokimbia na fedha za kampeni za Igunga.

Katika taarifa yake ya jana, Mtatiro alidai kuwa Septemba 20 mwaka 2011, wakati wa kampeni za Igunga, Kambaya alisaini Sh milioni 2.2 za kujikimu kwa ajili ya kusimamia mambo maalum waliyokubaliana kwenye zoni yake ya kampeni.

Mtatiro alidai kuwa Kambaya baada ya kusaini fedha hizo, alitokomea Dar es Salaam na kuitelekeza Zoni muhimu ya kampeni za Igunga bila kukiaga chama wala Katibu Mkuu, na hakurudi Igunga tena.

“Nilipokwenda kwenye Zoni husika baada ya siku tano, ndipo nakaambiwa Kambaya ametokomea. Ikabidi nimpigie simu hakupokea na nikachukua hatua za kumpandisha ndugu Mohammed Marjeby (aliyekuwa Mwenyeji wa Zoni) ili achukue nafasi ya Kambaya,”alidai.

Alidai baada ya Kambaya kutoroka na fedha hizo hadi leo, hakuwahi kuzirejesha na kwamba alichofanya ni kumjulisha Katibu Mkuu na Mwenyekiti.

Pia alidai kuwa hata mwaka juzi (wakati wa Uchaguzi Mkuu), Kambaya alipangiwa usimamizi wa kampeni katika maeneo kadhaa ya nchi, akakabidhiwa Sh. milioni 3 na hakwenda kwenye kampeni hizo.

Utetezi wa Mtatiro

“Wizi ni tabia tu na hata Kambaya akijaribu kuangusha mbingu ili Mtatiro nionekane mwizi atakuwa anamwaga maji baharini tu. Nina makubaliano ya kusimamia mambo makubwa maishani bila kujali nalipwa nini na bila kukubali kuhongwa.

“Kambaya akaulize namna nilivyosaidia maelfu ya wanafunzi wa vyuo vikuu vya Tanzania na wengine wakiwa hawana matumaini ya kupata mikopo kabisa, awaulize namna walivyoniletea malaki ya fedha za shukrani na sikuwahi kukubali kupokea hata senti tano yao. Tabia ya wizi ina minyororo yake na mimi Mtatiro sikuwahi kufikiria kuwa mwizi,”alisema.

Alihoji kuhusu Sh milioni 369, alizomtuhumu Kambaya kuwa alishiriki kuiba kimkakati kwa kusaidiana na Lipumba na kundi lao baada ya Januari 4 mwaka huu, ambapo Magdalena Sakaya, Thomas Malima na mwingine aliyetajwa kwa jina moja la Zainab, walifanywa watia saini wa akaunti ya wilaya ya CUF.

Mtatiro alidai kuwa baada ya Kambaya na wenzake kuchukua fedha hizo, walikwenda kwa Lipumba na kuanza kugawana, hivyo hapasawi kuzifananisha fedha halali za chama zilizotumwa Igunga kwa awamu na fedha hizo zilizochukuliwa Hazina kinyemela.

Mtatiro alisema wakati yeye anawekewa fedha zaidi ya Sh milioni 100 katika akaunti yake, kulikuwa na baraka ya Kamati ya Utendaji ya Taifa, Katibu Mkuu, Mwenyekiti Taifa na Kurugenzi ya Fedha kwa ajili ya kampeni za Igunga.

Alisisistiza kuwa hakukuwa na nia yoyote mbaya kwa chama kumwelekeza afungue akaunti na kisha kuiweka fedha kwa ajili ya bajeti ya kampeni kwa awamu.
Mtatiro alisisitiza kuwa yeye ni mtu wa kanuni na kwamba hawezi kuyumbishwa na wezi.

"Kimaadili mimi huwachukia wezi na waongo. Kwa sababu tunayo nafasi ya kuchukua hatua kwa kila mwizi, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, Bwaba Yule na wenzake. Hatua zitachukuliwa haraka sana," alisema.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo