Mizigo ya abiria yateketea moto uwanja wa ndege Dar


Salha Mohamed

Moto Uwanja wa Ndege JNIA
MOTO uliotokea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), umeteketeza chumba cha mizigo ya abiria cha uwanja huo na mizigo yote iliyokuwepo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alisema moto huo ulitokea usiku wa kuamkia jana saa tano usiku katika chumba kidogo cha kuhifadhia mizigo ya abiria cha kampuni Swissport, inayohudumia abiria.

Akizungumza mara baada ya kukagua eneo lililoteketea akitokea Mwanza, Mbarawa alisema tayari ameunda timu ya watu 12 ya kuchunguza chanzo cha moto huo ndani ya mwezi mmoja.

“Ukitokea moto watu watasema ni janga tu limetokea, lakini kuna uchunguzi wa kitaalamu kwanini moto umetokea na sisi tumeunda timu ya wataalamu wafanye uchunguzi wa kina kwa nini moto ule ulitokea,”alisema.

Alisema timu hiyo yenye watu 12 inaongozwa na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Makao Makuu (TAA), Joseph Nyahende ambayo anatarajia watatoa majibu ya uhakika.

“Tume hii watatoa majibu ya uhakika, hawatatupa bahati mbaya imetokea maana kwenye utaalamu hakuna kitu bahati mbaya kuna sababu ya msingi,”alisema na kuongeza kuwa anatarajia kupata taarifa ya kitaalamu itakayoeleza chanzo cha moto huo.

Kutokana na ajali hiyo, alisema Serikali imeweka mikakakti ya kuhakikisha viwanja vyote vya ndege hakutatokea majanga ya moto kama uliotokea hapo.

“Kazi tunayosubiri ya msingi ni kupata majibu ya wataalamu ili tuone tatizo lilikuwa nini na turekebishe matatizo yote na si hapa tu, bali viwanja vya ndege vyote Tanzania,”alisema.

Mbarawa alisema ni lazima Serikali ihakikishe kuwa majanga ya moto hayatokei kama lililotokea juzi.

Mbarawa aliongeza kuwa si sahihi kumnyooshea kidole mtu kutokana na moto huo kwa sasa, kwani si sahihi hivyo wasubiri taarifa ya wataalamu ili kuona kosa lilipo.

Aliongeza kuwa hadi sasa hawajui thamani halisi ya mizigo iliyoungua na nini kilikuwepo ndani ya mizigo hiyo kwani hawana mamlaka ya kuangalia kama abiria hayupo.

Katika hatua nyingine, mbarawa ametoa miezi miwili kwa kampuni ya kusafirisha mizigo ya Swissport kurekebisha utoaji huduma kwa abiria kwakuwa huduma zao haziridhishi.

“Swissport imekuwa ikifanya kazi peke yake kwa muda mrefu sana hapa uwanja wa ndege, hatuwezi kujua kama huduma zao ni mbaya lakini kwa taarifa nilizopata huduma haikidhi mahitaji,”alisema.

Alisema mwaka jana waliingiza kampuni nyingine ya Nas Dar Airco kufanya kazi, lakini haijafanya kazi huku ikidaiwa Swissport kuweka mazingira ya kampuni hiyo mpya kutofanya kazi.

Alisema tayari wameleta wataalamu wa kuangalia kama kampuni hiyo inafanya ujanja ujanja kinyume na taratibu za sheria yake.

“Kama anafanya ujanja ujanja wowote kinyume na leseni aliyopewa, lazima tutaifuta leseni, lazima ufanye kazi na kila mtu katika uwanja wa ndege huu umpe haki sawa…kama mlizoea hivyo wakati huu sio.

“Wakati umepita lazima mfanye kwa utaratibu na kanuni zilizowekwa, vinginevyo kama hamkufanya hivyo nikiletewa leseni mimi naifuta,”alisema.

Alisema anaamini ufanisi utakuwepo kama kutakuwa na kampuni nyingi zinazofanya kazi katika uwanja huo kwa kuwa baadhi ya mashirika ya ndege yameanza kulaumu huduma za Swissport.

“Nasema si kwa sababu ya moto lakini nasema kwa sababu awali huduma zako hazipo vizuri, watu wamelalamika sana tumekupa fursa tumia fursa vizuri tuwaletee wasafiri wetu huduma nzuri,”alisema.

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Swissport, Mrisho Yasin alisema tuhuma hizo ndiyo amezisikia kwa Waziri, hivyo watazifanyia kazi na kutoa mrejesho.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo