Lowassa: CCM inaweweseka na Ukawa


Mwandishi Wetu, Kahama 

Dk. John Magufuli
WAZIRI Mkuu wa zamani na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa, amesema CCM inatiwa kiwewe na kasi ya kuimarika kwa umoja na mshikamano wa vyama upinzani nchini.

Lowassa alitoa kauli hiyo jana alipozungumza mjini hapa akiwa njiani kuelekea Kagera kwa ziara ya kuimarisha chama.

Alisema kuimarika kwa mshikamano huo chini ya mwavuli wa UKAWA ni hatua kubwa katika kuelekea kuing'oa CCM madarakani.

“Wameanza mbinu za kutaka kutuondoa kwenye umoja wetu, wameanza kuwalisha viongozi wetu maneno, mfano gazeti… la Januari 12 walinilisha maneno kwamba eti nimeitabiria CCM ushindi katika uchaguzi mdogo wa udiwani Arumeru...hayo ni mambo ya ajabu kabisa, gazeti linaamua kutumika kuvunja demokrasia? Inasikitisha sana,” alisema Lowassa.

Lowassa aliyefuatana na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu alisema wananchi wameshajua mbinu chafu za CCM na hawako tayari kuona hamu yao ya mabadiliko inapotea.

Alisema viongozi wa vyama vya upinzani wako kwenye mshikamano mkubwa na kuwataka wanachama kuiga mfano huo.

“Katika ziara zetu hizi za kuimarisha chama pia tunaimarisha mshikamano miongoni mwetu wapinzani. CCM wanapata kiwewe na tunawaambia hata wafanyeje, mabadiliko hayaepukiki, watawatia ndani viongozi wetu kwa hila, lakini wajue hiyo ndiyo inazidisha vuguvugu, huu ni upepo unaovuma kote duniani hivi sasa wajifunze yaliyotokea Gambia, Ghana na kwingineko,” alisema Lowassa.

Lowassa na msafara wake walisalimiana na wananchi kwenye mnada wa Lusaunga, Biharamulo ambako wananchi hao walimwambia kuwa hali yao ya maisha ni ngumu kutokana na ukame unaowakabili.

Hata hivyo, Lowassa hakusema lolote zaidi ya kuwapungia na kuwasalimia akisema mikutano ya hadhara imepigwa marufuku na asingependa kuvunja sheria na amri hiyo hata kama ni kandamizi.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo