JPM: Lalamikeni tu mimi narekebisha nchi


Mwandishi Wetu
Rais John Magufuli

RAIS John Magufuli amesema hatua anazochukua kurekebisha nchi na kusababisha watu kulalamika hazitabadilika na msimamo wake uko palepale.

Kauli hiyo aliitoa juzi wakati wa uzinduzi wa barabara ya Bariadi- Lamadi mkoani Simiyu yenye urefu wa kilometa 71.8 ambayo itagharimu Sh bilioni 90 hadi kukamilika kwake.

Alisema cheo ni dhamana na kwamba mtu mwenye hofu ya Mungu lazima atekeleze alichoahidi, hivyo atahakikisha anatekeleza aliyoahidi licha ya baadhi ya watu kulalamika.

"Kwenye kila zuri lazima mabaya yawepo, nilisimamia kwenye ufisadi, wizi na mambo mbalimbali, lakini hatua hiyo imenifanya nichukiwe, naomba watambue kuwa mimi nazidi kusonga mbele kwa mbele ili kuleta maendeleo," alisisitiza.

Alisema mtendaji yoyote wa Bariadi atakayevuruga, asitarajie kuhamishiwa eneo lingine bali atambue kuwa atafia hapohapo alipoharibu.

Alisisitiza kuwa hatengenezi nchi ili kudhulumu mali za Watanzania wenye maisha duni na kwamba haiwezekani mtu mwingine ale mali za mwenzake.

Alisema Bariadi inaongoza kwa kuuza pamba, dhahabu, ina hifadhi ya Serengeti ambako watu wa Ulaya hufika kutazama wanyama, hivyo haiwezekani pamoja na rasilimali hizo nchi iwe masikini.

Rais alisema kwa kiasi kikubwa anapambana na wanaofanya nchi iwe masikini kwa kuwa hakuna mzee, kijana wala mtoto anayependa umasikini na kila mtu anapenda kupata mahitaji ya msingi.

Alisema kwenye bajeti ya Sh trilioni 29.5 asilimia 40 yake ni kwa ajili ya miradi ya miundombinu na haijawahi kutokea kiasi kikubwa hivyo cha fedha kupangwa kwani awali ilikuwa ni asilimia 26 tu.

“Kutokana na hilo kuna watu wamelalamika na wanazidi kulalamika na mnaosikia wanalalamika ndio walikuwa wanafaidi fedha hizo na walalamike sana, maana nataka ziende kwenye maendeleo ya Watanzania," alisema.

Alifafanua kuwa hadi sasa amenunua ndege sita na hakuna nchi iliyoweza kuleta watalii bila ndege zake, hivyo ameamua kuinua utalii ili ifikapo mwakani Bariadi iwe na uwanja mkubwa wa ndege.

Alisema kupitia fursa hizo, uchumi wa wana Bariadi utaimarika na wafanyabiashara   watafanya biashara zao vizuri na kujipatia kipato.

Aliongeza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha miradi ya barabara inaendelea na alimwagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ahakikishe eneo la kiliometa 51.3 lililobaki la barabara linajengwa haraka na la kilometa 48.9 litangaziwe zabuni ili nalo likamilike.

Alisema ujenzi wa barabara hiyo pia utasaidia magari yanayotoka Nairobi yaliyokuwa yanazunguka, kupita bila changamoto na kufika kirahisi huku akiasa madereva kuwa makini barabarani ili kuepuka ajali zisizotarajiwa.

Aliwataka wananchi wa Simiyu wasing’oe nati za madaraja, alama za barabarani, wasimwage mafuta kwenye barabara hizo ili zidumu kwa muda mrefu.

Akitoa maelezo ya awali, Profesa Mbarawa alisema kati ya Sh bilioni 90 zilizotumika kwenye ujenzi huo, Sh bilioni 80 ni za ujenzi, na zingine ni gharama mbalimbali zikiwamo za usimamizi, usanifu na fidia kwa wananchi waliobomolewa nyumba.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo