Waliomcharaza viboko mwanamke waachwa huru


Frankius Cleophace, Tarime

WATUHUMIWA 10 waliokamatwa juzi wakihusishwa na tukio la kumcharaza viboko hadharani mwanamke wameachwa huru na Jeshi la Polisi.

Watuhumiwa hao waliachwa huru asubuhi ya jana baada ya kukaa rumande kwa siku mbili.

Hata hivyo, haijafahamika sababu ya Polisi kuwaacha watuhumiwa hao kutokana na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya kushindwa kulizungumzia suala hilo hata alipotafutwa ofisini kwake ambapo alidai ana kazi ambayo ilitakiwa kufanywa kwa wakati huo na kushauri kuonwa kesho.

Baadhi ya wakazi wa Rorya ambao ni Wasimbiti, walisema adhabu iliyotolewa kwao ni ya kawaida kwa watu wenye tabia mbaya kwenye jamii yao. 

Mwita Wambura wa Nyamaguku alisema wazee hufikia kutoa adhabu kama hiyo kulingana na maelezo ya mtuhumiwa.
  
"Ni kawaida kwetu wazee wa Irienyi Ndodo kutoa adhabu kama hizo, maana kuna watu ni wakarofi sana, lakini wazee wanasaidia kuwanyoosha na kurejesha maadili kwenye jamii, na ndiyo maana hata aliyetendewa vile alishasahau na hakwenda kushitaki.

“Pia wazee wanapotoa adhabu kama hiyo, huandika taarifa na sababu ya kufanya hivyo, hivyo walikuwa sahihi," alisema Wambura.

Aliitaka Serikali kuwapa nguvu wazee hao ili waendelee kusimamia maadili katika kabila lao, kwani wakiacha kusimama kidete hali ya usalama itakuwa mbaya.

Hata hivyo, Rose Mwita alipingana na msimamo wa Wambura kwa kudai kuwa haikuwa halali kutoa adhabu kubwa kiasi kile hadi kumwacha uchi mama huyo mwenye umri wa miaka 38 mkazi wa kijiji cha Kinesi, Rorya.
  
Tukio la kucharazwa viboko kwa mama huyo lilifanyika Januari 23 mwaka jana, lakini lilikuja kufahamika Januari 9 mwaka huu baada ya kurushwa mitandaoni.

Hata hivyo, kijana aliyerusha video hiyo kwenye mitandao ya kijamii, anakabiliwa na adhabu ya wazee wa kimila ambao walisema alikiuka maadili ya kabila hilo.

Anaweza kutengwa na jamii, kwa kipindi fulani asisalimiane nayo, au asinywe pombe kokote au kuchapwa viboko.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo