Wakulima, wafugaji waomba mawaziri 3 wasuluhishe


Salha Mohamed

WAKULIMA na wafugaji mkoani Morogoro wamewataka mawaziri watatu kufika mkoani humo ili kutafuta suluhu ya migogoro yao.

Mawaziri hao ni wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, wa Kilimo na Chakula, Charles Tizeba na wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba.

Hatua ya wakulima na wafugaji hao ilifikiwa baada ya kuwa na migogoro yenye madhara kwa kusababisha vifo vya watu na mifugo na uharibifu wa mazao.

Wakizungumzia changamoto na migogoro wanayopata wafugaji mkoani humo juzi kupitia Kituo cha Televisheni cha Clouds katika kipindi cha Clouds 360, walisema chanzo cha migogoro hiyo ni mipaka, huku Serikali ikishindwa kuwasaidia.

Mmoja wa wafugaji mkoani Morogoro, Kalaita Motosya alisema migogoro mingi inayotokea mkoani humo husababishwa na ardhi kutokana na kutokujua mipaka yao.

Motosya ambaye ana ng’ombe 200 alisema maeneo yaliyotengwa na Serikali kwa ajili ya wafugaji ni machache ikilinganishwa na idadi ya wafugaji walio kwenye maeneo hayo.

“Maeneo yenye mgogoro Serikali ilivuruga mpango halali wa vijiji na kudai vipo vilivyoanzishwa vibaya na kudai kutafuta mwekezaji,” alisema.

Alisema kutokana na wafugaji kutafuta malisho hasa nyakati za kiangazi, hukimbilia sehemu zenye maji ili kunywesha mifugo yao ndipo hukutana na wakulima wakiwa maeneo hayo ndipo mgogoro unapoanza.

Alisema kila binadamu ana asili ya kibinadamu, hivyo mfugaji anaweza kuingiza mifugo kwenye shamba la mkulima kwa bahati mbaya au kuzidiwa na idadi ya ng’ombe.

Akizungumzia hali hiyo, mmoja wa wakulima mkoani humo, Bakari Shafii alisema wafugaji wamekuwa wakiingiza ng’ombe kwenye mashamba yao kwa makusudi na pindi wanapobaini huambiwa waachwe ng’ombe wale.

“Ukikuta ng’ombe shambani, ukimfuata mfugaji na kushauriana kuwatoa labda wamemshinda, hukwambia waache kwani mazao yana gharama gani,” alisema.

Alisema inapofikia hatua hiyo, mkulima anapobaini kupata shida wakati akilima ndipo suala la kushambulia mifugo hujitokeza baada ya wafugaji kukaidi kutoa ng’ombe mashambani.

Alisema wamechoka kuuawa na wafugaji, kwani wengi wamekuwa wakichukua sheria mkononi huku wafugaji wakiwadharau.

Kutokana na hali hiyo, Shafii alitaka mawaziri hao kukutana ili kupata suluhu ya mgogoro ambao unahatarisha maisha yao.

Motosya aliitaka Serikali pia kuboresha miundombinu ya wafugaji kama kutengeneza vyanzo vya maji na maeneo ya malisho ili wafuge kisasa.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo