Mgogoro wafukuta CCM Singida


Mwandishi Wetu

Martha Mlata
MBUNGE wa Viti Maalumu na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Singida, Martha Mlata, anatuhumiwa kutengua uamuzi wa Baraza la Madiwani la Novemba 28 mwaka jana na kuridhiwa na Kamati ya Siasa ya CCM ya Wilaya ya Singida, kuhusu mahali makao makuu ya wilaya hiyo yatakapojengwa.

Mlata pamoja na kada mwingine wa CCM na Mbunge (Jina lake linahifadhiwa) wanatuhumiwa   kuingilia utendaji na kutengua uamuzi halali wa madiwani.

Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili jana, Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Singida, Naruma Hanje alisema Mlata amekuwa haridhiki na nafasi aliyonayo, kwani anataka kuwa Mwenyekiti wa Mkoa na wa Wilaya zote, ili afanye uamuzi bila maelekezo kutoka kwa wenyeviti wa wilaya.

“Mimi nimesikia ameagiza niwaandikie barua madiwani ambao hawakuhudhuria mkutano wake wajieleze, lakini siwezi kufanya hivyo kwa kuwa hawana kosa, wanafanya kazi na waliamua eneo la kujenga Halmashauri kwa kikao halali kisheria, Mlata analeta vurugu tu,” alisema Hanje.

“CCM tuna utaratibu wetu, mtu akikosea huitwa kuonywa, lakini Mlata alifika Ilongero na (Mbunge) na kutoa matusi hadharani, hawa ni watoto wetu tumewalea, wametuvunjia heshima kabisa,” alisema.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Elia Digha alipopigiwa simu kuulizwa kama ana taarifa ya jambo hilo alisema: “Najua na naamini madiwani hawakukosea, walifuata sheria, kinachofanywa na Mlata na … ni kujitoa ufahamu kwa jambo ambalo liko wazi.”

Alisema Serikali inawataka wajenge Halmashauri kwenye maeneo ya wazi ambako hawatatumia fedha nyingi kulipa fidia, lakini Mlata na mwenzake wamekuwa wakishirikiana na kikundi kidogo ambacho hata si sehemu ya madiwani kufanyia fujo madiwani.

Alisema baada ya kina Mlata kufika Ilongero Januari 7, waliwatangazia wananchi kuwa eneo hilo litakuwa wilaya kabla halijatangazwa kisheria na matokeo yake waliwaondoa kwa nguvu viongozi wa CCM wa wilaya kwenye jengo la Singida mjini bila makubaliano.

Digha alifafanua kuwa Kamati ya Siasa ya CCM ya Wilaya hiyo chini ya Hanje, ilipewa mapendekezo na wataalamu juu ya umuhimu wa kujenga makazi hayo Kinyamwambo badala ya Ilongero na ikakubaliana kwa sababu za kiuchumi.

Mwenyekiti huyo alisema Oktoba 20, 2014 katika muhtasari namba 42/2014, wa Baraza la Madiwani chini ya Juma Samwi, Diwani wa zamani wa Ilongero alihudhuria.  

“Sisi madiwani tulifuata taratibu na sheria, Mkuu wa Mkoa aliyeondoka alikuwa hafuati sheria, anatuvuruga, anakivuruga chama chetu sababu maazimio haya ya madiwani yalikubaliwa pia na Kamati ya Siasa ya CCM ya Wilaya, Septemba 28 mwaka jana, kikao cha kamati ya uongozi kiliridhia, kikifuatiwa na kikao cha kamati ya kudumu ya uchumi na fedha cha Novemba 13   ambacho kilitoa mapendekezo kwenye Baraza,” alisema Digha.

“Hata kamati ya chama ya madiwani wa CCM ilikubali, na kikao hicho kilikuwa na madiwani 29 na wote waliridhia, hadi kupelekea Baraza halali la madiwani Oktoba 28 mwaka jana kupitisha maazimio kuwa makao makuu yajengwe Kinyamwambo badala ya Ilongero,” alisema.

Akijibu tuhuma hizo Mlata alisema hazina ukweli na kuwa wanaomtangazia sifa mbaya wataumbuka kutokana na kukosa hoja za msingi.

“Waambie wafuate taratibu za chama, kufikisha malalamiko yao wanatakiwa kutambua kuwa mimi ni bosi wao kichama, hivyo siko tayari kuona ukiukwaji unatokea nikanyamaza,” alisema.

Mwenyekiti huyo alisema wanaolalamika ndio wavunja nchi na wanapaswa ‘kutumbuliwa’, kwa kuwa ni ‘majipu’ kwenye mkoa na wilaya hiyo ambayo ipo kwenye mchakato wa kupiga hatua za kimaendeleo.

Alisema kwa upande wake hana maslahi yoyote anayopigania katika suala hilo, hivyo ni jambo la kusikitisha yeye kuhusishwa.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo