Watalamu wa kilimo saidieni kukomesha njaa – Mghwira


Badrudin Yahaya

Anna Mghwira
MWENYEKITI wa Chama cha ACT - Wazelendo, Anna Mghwira, amewashauri wataalamu wa masuala ya kilimo nchini kuwapa njia bora wakulima ili wapate mazao ya kutosha badala ya kuwashawishi watumie mbegu za kisasa pekee.

Mghwira amesema mbegu nyingi za kisasa zinazotengenezwa viwandani na kuuzwa kwa ajili ya shughuli za kilimo hazina ubora hata wa kuishi katika misimu miwili ya kilimo, hivyo kuwafanya wakulima kulazimika kununua mbegu kila msimu wa kilimo unapofika.

Alisema hayo katika mdahalo maalumu wa kipindi cha Morning Trumpet kinachorushwa na runinga ya Azam Two alipokuwa na Mratibu wa Mtandao wa Baionaia, Abdallah Ramadhan.

Walikuwa wanazungumzia tatizo la njaa ambalo limeanza kutokea katika baadhi ya maeneo ya nchi na kuanza kutishia amani.

“Kinachotatiza nchini kwasasa hadi kufikia hatua ya kuelekea katika baa la njaa ni kwamba wataalamu wamekuwa wakilazimisha wakulima watumie mbegu za viwandani, lakini mbegu hizo hazina ubora ambao unatakiwa na hivyo ni vyema tukatumia mbegu za asili tu,” alisema.

Kwa mujibu wa mgombea huyo wa urais wa mwaka 2015, wataalamu wanatakiwa kufanya tafiti za kutosha na kuwapatia ufumbuzi wakulima wa kuhusu namna ya kulima kwa kutumia mbegu asili bila kupata matatizo.

Aliwanyooshea kidole wananchi kuhusu hali ya mabadiliko ya tabia ya nchi akisema wanahusika kwa asilimia kubwa wa kulipelekea Taifa katika hali ya kuwa jangwa kutokana na ukosefu wa mvua kwa muda mwafaka.

Alishauri wananchi kutafuta namna nyingine ya nishati na si kuendelea kukataa miti kwaajili ya kuchomea mkaa kitu ambacho kinapelekea kuteketeza misitu.

Kwa upande wake, Ramadhan alisema kuwa matumizi ya mbegu za kisasa yana faida kubwa ikiwamo usalama, kwani kuna mbegu za aina nyingi zikiwemo zile za kustahamili ukame ambao au ukosefu wa mvua kwa kipindi kirefu kama ilivyo hivi sasa nchini.

Mratibu huyo pia alisema katika hali ya kukabiliana na njaa wakulima wanatakiwa kubadili mawazo yao ya kuzalisha mazao ya aina moja na hivyo waanze kujenga tabia ya kuwa wanachanganya mazao ya aina tofauti ili hata ikitokea madhara basi wasikose kabisa hata chakula kidogo.

“Ili kukabiliana na hali ya njaa ambayo inalikabili taifa kwasasa basi ni vyema wakulima wetu wakaweka tabia ya kuchanganya mazao tofauti shambani ili wasije wakakosa kitu cha kuvuna,” alisema.

Alisema kuwa mbali na aina hiyo ya kilimo kuwa itasaidia katika kuwapatia mazao wananchi lakini pia njia hiyo inasaidia kutunza ardhi.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo